Afisa wa masoko kutoka ALAF Ltd. Bi. Theresia Mmasy akielezea jinsi Tuzo za Raisi za Mzalishaji Bora wa Viwanda(PMAYA) zilivyo za haki na huru.
Waandishi mbalimbali walioshiriki katika kuunga mkono uzinduzi wa shindano la 15 la Tuzo za Raisi za Mzalishaji bora wa mwaka(PMAYA)Afisa wa masoko kutoka ALAF Ltd. Bi. Theresia Mmasy akielezea jinsi Tuzo za Raisi za Mzalishaji Bora wa Viwanda(PMAYA) zilivyo za haki na huru. Waandishi mbalimbali walioshiriki katika kuunga mkono uzinduzi wa shindano la 15 la Tuzo za Raisi za Mzalishaji bora wa mwaka(PMAYA)
Mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Bwana. Leodegar Tenga akisisitiza ushiriki wa viwanda vidogo na vya kati kushiriki katika mashindano ya Tuzo za Raisi za Mzalishaji Bora (PMAYA)
*************************************
Dar Es Salaam, Septemba 23 2020.
Kwa miaka 15 mfululizo, shindano la tuzo la Rais za mzalishaji bora wa mwaka wa viwandani linalofanyika kila mwaka maarufu kama “PMAYA” limepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Dhumuni la shindano la PMAYA ni kutambua makampuni yanayojihusisha na uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini Tanzania katika sekta mbalimbali kwenye vipengele vya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.
Akitangaza rasmi shindano la PMAYA kwa mwaka huu wa 2020, mkurugenzi wa Shirikisho la viwanda Tanzania (CTI) Bw. Leodegar Tenga alikaribisha viwanda kushiriki na kuungana na mlezi wa Shirikisho la viwanda Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Joseph Magufuli katika jitihada zake za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kwa kipindi chote tumepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali, na kwa mwaka huu tumekwisha pokea idadi kubwa ya washiriki kutoka viwanda mbalimbali kote nchini. Tunahamasisha makampuni mengi ya uzalishaji kushiriki na hususani tunahamasisha ushiriki wa viwanda vya kati na vidogo” alisema Bw. Tenga.
“Mbuyu ulianza kama mchicha , hivyo ni muda mwafaka kwa viwanda vya kati na vidogo kutumia jukwaa hili kama nafasi kwao kuongoza kwenye nyanja tofauti, kutambulika, kuchangia ukuaji wa biashara zao na kutambulika” aliongeza Bw. Tenga.
Shindano la PMAYA linaloandaliwa kwa heshima ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania akiwa kama mlezi wa Shirikisho la viwanda Tanzania, linadhamiria kutambua mchango wa sekta ya viwanda , kutangaza umuhimu wa sekta ya viwanda nchini, kuongeza tija kwenye viwango vya ufanyaji biashara pamoja na kukuza utawala bora wa makampuni nchini.
Meneja masoko wa kampuni ya ALAF Ltd iliyokuwa mshindi wa kiwango kikubwa kwenye kipengele cha chuma na bidhaa za chuma kwenye shindano la mwaka jana Bi. Theresia Mmasy alisema, “ALAF imekua ikishiriki kwenye PMAYA na tumekua washindi wa vipengele mbalimbali kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo kwenye kipengele cha chuma na bidhaa za chuma.
Kwetu ALAF tumeona umuhimu wa PMAYA na ni kwa sababu taratibu zote za ushiriki na mchakato wa kutafuta washindi unafanyika kwa haki na huru jambo linalotoa nafasi sawa kwa kila mshiriki kushinda. Sambamba na hilo, PMAYA ndio tuzo pekee za viwanda ambapo makampuni ya uzalishaji yanapata kutambulika.
Nayasihi makampuni mengine kuchangamkia fursa hii na kushiriki waweze kushinda.
Mashindano ya PMAYA yamekuwa moja ya njia fasaha kwa makampuni kuongeza ubora wa bidhaa na huduma zao kwa jamii. Tathmini ya shindano inafanywa na jopo huru la wakaguzi, na mwishoni hutoa taarifa na majibu ya tathmini iliyofanywa.
Washiriki hupewa taarifa ya tathmini ili waweze kufahamu mapungufu na umahiri wao kiutendaji kwa maendeleo yao kama kampuni
Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya PLASCO Ltd waliokua washindi kiwango kikubwa kwenye kipengele cha plastiki na mipira, meneja wa masoko na mauzo Bi. Edith James alisema,”Tuzo za PMAYA zimetoa fursa nzuri na ya kipekee kwa viwanda vya ndani. Zimesaidia pia katika kukuza ufahamu juu ya umuhimu wa kuhakikisha ubora kwenye sekta zote kwa mtazamo wa kuhamasisha mchango wa viwanda vya ndani kwenye miradi mikubwa ya miundombinu. Kampuni ya PLASCO imekua ikishiriki kwenye mashindano haya ya PMAYA na tumekuwa washindi katika vipengele mbalimbali jambo linalotupa nafasi kuongoza na pia kukuza biashara yetu. Nahamisisha Viwanda vyote Tanzania haswa ya kati na vidogo kushiriki na kuitumia kwa ufasaha nafasi hii kujitangaza kibiashara”
Uzinduzi wa shindano hili linafungua milango kwa wadau mbalimbali kwenye sekta ya viwanda kujisajili ili kushiriki kwenye shindano hili. Kujisajili tafadhali tembelea toviti ya shirikisho www.cti.co.tz. Mwisho wa kuwasilisha maombi ya kushiriki ni tarehe 12 Oktoba 2020.
Tuzo za Rais za mzalishaji bora wa viwandani PMAYA mwaka huu zinaandaliwa na Shirikisho la viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na GIZ – Kuunda mitazamo: kwa maendeleo ya Afrika Mashariki
Social Plugin