ASKARI wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wilayani Pangani wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 32 waliokutwa wakiwa karibu na hifadhi hiyo wakisafirishwa kupelekwa nchi za kusini mwa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa wahamiaji hao Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani Grace Lobora alisema kwamba wahamiaji hao walikamatwa Septemba 27 mwaka huu usiku.
Alisema ukamatwa huo waliofanya baada ya kupata taarifa kutoka wananchi wa Kijiji cha Buyuni kupitia Mwenyekiti wa Kijiji hicho Diwani Akida ambaye aliwaeleza uwepo wa mazingira yasiyoridhisha kwenye eneo lake hasa eneo la bahari baada ya boti moja kukwama.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo wao kama wahifadhi wana jukumu la kulinda maliasili na kuangalia usalama kwenye miji yote inayowazunguka waliandaa kikosi kazi cha kwanza waliokwenda eneo la tukio na walipofika waliwakuta wahamiaji hao eneo la bahari karibu na hifadhi hiyo katika kijiji cha Buyuni.
Alisema baadae hapo waliamua kutuma kikosi cha pili na ndipo walipofika na kufanikiwa kukaweka chini ya ulinzi wahamiaji 28 ambao ni raia wa Ethiopia lakini alfarji wakapata taarifa nyingine ya uwepo wa wahamiaji wengine wanne ambao ni raia wa Somalia na wakatuma kikosi na kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi.
“Kati yao wapo wahamiaji 32 raia wa Ethiopia 28 na raia wa Somalia wanne akiwemo mwanamke mmoja kwa hiyo baada ya kufanikisha tukio hilo tumewafikisha na kuwakabidhi kwenye mamlaka ya Polisi kwa ajili ya hatua zaidi”Alisema
Awali akizungumza kuhusiana na tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Blasius Chatanda aliwapongeza askari wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kazi nzuri kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Polisi wilaya ya Pangani.
Hata hivyo amesema kwamba hivi sasa wametangaza vita mpya kwa mawakala wanaojishuhulisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu mkoani Tanga kwamba hawatasalimika watasakwa popote iwe ni nchi kavu, majini na kisha kufikishwa mahakamani.
Social Plugin