MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Singida waingie kwenye kilimo cha kisasa ili waweze kuinua uchumi wao.
“Wananchi ingieni kwenye kilimo cha Kisasa na chenye tija ili muinue kipato chenu. Hili eneo la Gumanga ni zuri sasa kwa kilimo na wengi wenu wanalima mbogamboga. Vijana msikae kusubiri ajira za ofisini, ajira siyo lazima ukae ofisini, unaweza kujiajiri kwenye kilimo,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 15, 2020) wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Bw. Francis Isack Mtinga na mgombea udiwani, Bw. James Mkwega uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya mabasi Gumanga, wilayani Mkalama, mkoani Singida.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Singida kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alisema Serikali inatekeleza kwa vitendo ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 na moja ya mkakati wake ni kutoa fursa tofauti ili wananchi waweze kunufaika.
“Huku Singida ni wakulima wazuri wa alizeti na mna viwanda vingi vya kusindika mafuta. Tumieni fursa hii ya kilimo kuinua kipato chenu, Serikali yenu itaendelea kuboresha fursa za uwekezaji.”
Mapema, mgombea ubunge wa jimbo la Iramba Magharibi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba aliwataka wakazi wa Singida wasifanye mzaha kwenye masuala ya uchumi.
“Tuache mzahamzaha katika masuala ya uchumi na maendeleo na siku ya tarehe 28 Oktoba, tufuatane wote tukapige kura kwa Dkt. John Pombe Magufuli. Raha ya ushindi ni kuwa na kura nyingi za Rais, Wabunge na madiwani,” alisema.
Naye mbunge aliyemaliza muda wake, Bw. Allan Kiula aliahidi kusaidiana na Bw. Mtinga kufanya kampeni ili kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinapata ushindi mkubwa.
“Tutasaidiana na Bw. Francis Isack kutafuta kura za CCM. Tutafanya hivyo pia kwa ajili ya kura za madiwani wetu. Tunahitaji madiwani wa kutosha ili Bw. Isack aweze kupata timu ya kufanya nayo kazi kwa urahisi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza ekari 2,500 kati ya ekari 5,432 zilizoko kwenye kijiji cha Sagala zirejeshwe kwa wananchi ili zitumike kwa kilimo.
“Tunaboresha uchumi ili ushuke kwa wananchi iwe kwenye kilimo, uvuvi au ufugaji. Nina taarifa kuwa Halmshauri ya Singida kwenye Kijiji cha Sagala wamechukua ekari 5,432 na kuamua kuzikodisha kwa wannchi wakidai kuwa ni kitega uchumi cha Halmashauri.”
“Wao hawalimi, na kama hawana cha kufanya kwenye eneo lile, walirudishe kwa wananchi. Mkuu wa Mkoa wa Singida, uende kule na uanze mchakato wa kupunguza eneo hilo ili yapatikane mashamba ya kuwagawia wananchi. Nasikia wanawakodisha kwa sh. 50,000.”
“Najua hawawezi kulima ekari zote 5,000. Nenda kawapunguzie ekari 2,500 ili wagawiwe wananchi. Ingekuwa mjini hapa Ilongero, tungesema wanataka kupima viwanja na ningewasamehe, lakini kule ni mbali lazima warudishe hilo eneo kwa wananchi,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.
Aliwataka wananchi hao watakapopatiwa eneo hilo, walime kwa bidii ili mazao yao yaweze kuuzwa mjini na kwenye kata ya Ilongero.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin