Mratibu wa Mradi wa Wanawake na Uongozi unaotekelezwa na TGNP kwa kushirikiana na WILDAF na UN Women, Grace Kisetu
Kulia ni Mwezeshaji/Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Eva Hawa akizungumza wakati wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge Anjelina Mahona
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Uongozi siyo misuli bali ni busara na hekima ambazo hata mwanamke anazo!! Hii ni kauli ya baadhi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wakielezea namna walivyojinasua katika mfumo dume uliokuwa unamtazama mwanamke kuwa hawezi kuwa kiongozi.
Katika mchakato wa uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2020 jumla ya wanawake 61 wamejitokeza kugombea ubunge na udiwani Jimbo la Kishapu huku wagombea wengi wakitoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vyama vingine vya siasa havikusimamisha wagombea wanawake.
Kwa Mujibu wa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kishapu, Hellena Chacha jumla ya wanawake 52 walitia nia kuwania Ubunge na Udiwani katika Jimbo la Kishapu ambapo kati yao wawili wanagombea udiwani kata ya Mwakipoya na Idukilo na wengine 10 wameteuliwa kugombea udiwani viti maalumu.
Naye Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilaya ya Kishapu Castor Manyesha, anasema wanawake 9 walitia nia kuwania udiwani ambapo mmoja ameteuliwa kugombea ubunge kata ya Songwa hivyo kufanya idadi ya wanawake waliojitokeza kugombea ubunge na udiwani katika jimbo la Kishapu kuwa 61.
Josephine Malima ambaye ni miongoni mwa wagombea udiwani viti maalumu kata ya Ukenyenge kupitia CCM anasema mafunzo yanayotolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuhusu Ushiriki wa wanawake katika uongozi yamewasaidia wanawake kujitambua na kuona kuwa wanayo nafasi ya kuwa viongozi kama wanaume.
“Wanawake sasa tumejitambua na tumetambua kuwa Uongozi siyo misuli bali ni busara na hekima ambazo hata mwanamke anazo ndiyo maana sasa tunajitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwani tuna sifa za kuwa viongozi kama walivyo wanaume”,anasema Josephina.
Josephina anaipongeza jamii kwa kuondokana na mitazamo hasi kuhusu wanawake kuwa viongozi ambapo sasa hata wanaume wameielewa nguvu ya mwanamke na wamekuwa wakiwaruhusu wake zao kuchukua fomu kuwania nafasi za uongozi lakini pia wamekuwa wakiwapa ushirikiano hadi katika kampeni.
Hata hivyo ameishukuru TGNP kwa mafunzo ya wanawake na uongozi ambapo wanawake wengi wamejengewa uwezo kuhusu masuala ya uongozi ambayo yamewajengea hali ya kujiamini na kutawala majukwaa ya kisiasa.
Anjelina Mahona (31) ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge aliyeanza kuwania uongozi mwaka 2011 akiwa ni binti mwenye umri wa miaka 22 tu anasema kutokana na kuwa na dhamira ya kuwa kiongozi na kujiamini kwake kuwa anaweza kuwa kiongozi mwanamke,Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bulimba.
"Nguvu ya kujiamini na kujitambua zaidi iliongezeka maradufu mwaka 2015 baada ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kufika wilayani Kishapu na kutoa elimu ya uraghbishi na mafunzo mbalimbali kuhusu haki ya mwanamke",anaeleza Anjelina.
“Kupitia ujuzi na elimu tuliyopatiwa kuhusu haki za wanawake,nilifanikiwa kujisimamia na kuwashauri wanawake wenzangu njia za kuondokana na maisha tegemezi na kumtoa mtu katika hali ya chini na kukabiliana na mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke. Mwaka 2019 nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola",anasema Anjelina.
Anjelina anasema kupitia uenyekiti wake wanawake wengi wameanza kujitokeza kugombea nafasi za uongozi mfano katika kijiji cha Bulimba kabla ya mwaka 2011 hadi 2015 wanawake viongozi walikuwa wawili tu lakini sasa wapo wanne.
“Nashukuru wanawake tunazidi kujitokeza kugombea na kushika nafasi za uongozi na jamii inaendelea kutumiani na kutuunga mkono. Leo hii kwa jinsi jamii inavyouamini uongozi wangu hata nikitaka kugombea udiwani naweza maana sifa za uongozi ninazo.Mimi nimeanzia chini nitaendelea kupanda”,anasema.
Katibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya ya Kishapu, Peter Nestory anasema kabla ya mafunzo ya wanawake na uongozi hapakuwa na viongozi wanawake wa kuchaguliwa wilayani Kishapu zaidi ya wale wajumbe wa kuteuliwa katika ngazi ya vitongoji,vijiji,kata na wilaya lakini sasa mambo yamebadilika.
“Mfano katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 wanawake wengi walijitokeza kugombea nafasi za uongozi. Esther Kweji Lugondeka alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Nshishinulu kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge,Anjelina Mahona akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge”,amefafanua Nestory.
Nestory anaeleza kuwa mbali na Esther Kweji Lugondeka na Anjelina Mahona, mnufaika mwingine wa Mafunzo ya Mwanamke na Uongozi yaliyotolewa na TGNP ni Josephina Malima ambaye mwaka 2015 alichaguliwa kuwa diwani wa viti maalumu kata ya Ukenyenge na sasa katika uchaguzi mkuu 2020 anagombea tena udiwani viti maalumu kata ya Ukenyenge.
Nestory anasema licha ya wanawake wengi kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, pia hivi sasa wanawake wanahudhuria kwa wingi kwenye vikao na mikutano na wamekuwa na ujasiri wa kuhoji badala ya kukaa kimya kwa mambo yanayohusu maendelo ya jamii na hata kwenye Mabaraza ya wazee wa mila wamekuwa wakikaribishwa kama wajumbe.
“Jamii imewatambua wanawake kuwa ni viongozi wazuri, imewathamini na imeacha kutumia maneno ya kuwakejeli. Mitazamo hasi imepungua na wanaume wanaruhusu wake zao kugombea nafasi za uongozi”,ameongeza Nestory.
Kwa upande wake, Mwezeshaji kutoka TGNP Eva Hawa Juma anasema mila na desturi zinazokandamiza mwanamke zimepungua wilayani Kishapu ambapo sasa wanawake wanashiriki katika shughuli za maendeleo na wamekuwa wakitoa maoni kwenye mikutano na vikao.
“Kwa kweli yapo mabadiliko yanayoonekana,mitazamo hasi dhidi ya wanawake na mila kandamizi zimepungua ambapo sasa jamii inahubiri ‘Mwanamke Anaweza’ na wanaume wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa wanawake wenye uthubutu wa kugombea nafasi za uongozi”,ameongeza Eva Hawa.
Mratibu wa Mradi wa Wanawake na Uongozi unaotekelezwa na TGNP kwa kushirikiana na WILDAF na UN Women, Grace Kisetu amesema michakato ya kubadili mitazamo hasi dhidi ya wanawake sasa imekuwa sehemu ya maisha ya jamii.
“Mradi huu ulioanza mwaka 2018 na kutarajiwa kufikia kikomo Septemba 2020,unaotekelezwa katika wilaya ya Kishapu (Shinyanga), Tarime (Mara), Kasulu (Kigoma) na Meatu (Simiyu) una lengo la kuhakikisha jamii inamkubali mwanamke kama kiongozi bora hasa katika siasa”,ameeleza Grace.
Amesema licha ya kuhamasisha jamii kuachana na mitazamo hasi na mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke,TGNP imewajengea uwezo wanawake kuhusu masuala ya uongozi ili washiriki katika siasa.
“Tumetengeneza mitandao na vikundi kwa ajili ya vuguvugu la harakati za ukombozi wa wanawake (Ujenzi wa nguvu ya pamoja -TAPO) katika maeneo yote tunapotekeleza mradi wa Mwanamke na Uongozi. Tuna vituo vya taarifa na maarifa Kasulu na Tarime na mtandao wa Nyuki Kishapu na Siafu Meatu na tumefanikiwa kuwafikia moja kwa moja wanaharakati takribani 1000”,amefafanua Grace.
“TGNP imefanikiwa kuionesha jamii kuwa wanawake wanaweza ili kufikia usawa wa kijinsia hivyo wapewe nafasi za uongozi ili kuleta maendeleo katika jamii”,amesema.
Hata hivyo amebainisha kuwa rasilimali fedha ni miongoni mwa changamoto inayosababisha TGNP ishindwe kuwafikia wananchi wengi zaidi kwani bado kuna mitazamo hasi katika jamii kwamba mabadiliko yanahitaji.
“Naomba jamii ibadilike kwani siyo kila mabadiliko yanahitaji fedha. Kila mmoja katika jamii anayo nafasi ya kuhamasisha kuondokana na mitazamo hasi na kuachana na mila na desturi zinazokandamiza mwanamke”,amesema Grace.