Her Initiative inatoa elimu ya dhana nzima ya masoko mtandaoni na namna ya kufanya biashara kwa ufanisi mtandaoni.
Changamoto katika biashara ni nyingi na hutokea mara nyingi, lakini changamoto inayoweza kumrudisha nyuma mfanyabiashara ni ile ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na mauzo yake au upatikanaji wa wateja katika huduma ama bidhaa yake.
Kezia ni mfanyabiashara wa viazi anasafirisha kutoka mbeya kwenda Dar es Salaam kuuzia wafanyabiashara wa chips, mfanyabiashara huyu ni kati ya wafanyabiashara wengi wanaoathirika na waliothirika na milipuko wa majanga mbalimbali katika jamii.
“Baada ya Corona kuingia hofu ilitanda kwa upande wangu na pia kwa walengwa wangu (wateja), ikapelekea biashara yangu kuyumba sana maana ilinihitaji kusafiri hivyo ikishindikana. Niliokuwa nawapelekea mzigo nao waliyumba kiuchumi, kila kukicha ilikua afadhali ya jana. Mtaji wangu ulizidi kupotea na kilichonisukuma zaidi ni wakati nilipokua naperuzi mtandaoni nakuona wafanyabiashara wenzangu wakiendelea na biashara. Hivyo baada ya corona nikaamua njia nzuri ya biashara yangu ni kuifanya asilimia 80% mtandaoni.” Kezia (Mnufaika wa Mradi wa Naimarika).
Nchini Tanzania asilimia 51 ya wanawake wanafanya biashara katika sekta isiyo rasmi hutegemea msongamano kwa watu ili kupata wateja wa bidhaa na huduma zao. Kutokea kwa majanga mbalimbali kama mlipuko wa Covid-19, wafanyabiashara wengi huathirika kutokana na hatua elekezi za kujikinga na kuepuka majanga hayo. Kupungua kwa msongamano wa watu ni kati ya hatua elekezi iliyosababisha changamoto ya mauzo kushuka kwa wafanyabiashara wengi nchini hasa walio katika sekta zisiszo rasmi.
Her Initiative kupitia mradi wake wa IMARIKA unaofadhiliwa na shirika la Women Fund Tanzania meandaa programu maalumu ya wasichana wafanyabiashara kuanzia miaka 18-30 kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizojitokeza kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Programu hii maalumu ina lengo la kuwaongezea wasichana wajasiriamali utaalamu wa namna ya kukabiliana na madhara ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Mradi wa IMARIKA umelenga kuwasaidia wajasiriamali wasichana kutunza afya zao za akili, kujenga ujasiri wa kukataa ukatili wa kijinsia na mafunzo ya elimu ya masoko mtandaoni ili kuwawezesha kukabiliana na chamgamoto zinazoawaathiri kipindi cha majanga yanapotokea.
Moja ya wanufaika wa mafunzo ya masoko mtandaoni akiwa ameshikilia bango linaloonesha ujumbe alioandaa kuhusu biashara yake baada ya mafunzo.
Kupitia mafunzo ya elimu ya masoko mtandaoni, Her Initiative inatoa elimu ya dhana nzima ya masoko mtandaoni na namna ya kufanya biashara kwa ufanisi mtandaoni. Baadhi ya mambo muhimu wanayojifunza wanufaika wa mafunzi hayo ni pamoja na umuhimu wa kuwa na mkakati wa masoko, mpango wa kuandaa maudhui, uundaji wa chapa (branding) ya biashara au huduma pamoja na mbinu za kukuza masoko mtandaoni.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa njia ya mtandao yamelenga kuwafikia wasichana wajasiriamali 300. Sambamba na mafunzo hayo wanufaika wanapata nafasi ya kupata ushauri wa masoko kutoka kwa wataalamu wa biashara na masoko mtandaoni. Pia baada ya kukamilisha mafunzo ya siku tatu wasichana wanapata vyeti vya ushiriki na washiriki 50 bora wanaofaulu jaribio linalofanyika baada ya mafunzo kupata zawadi ya kulipiwa tangazo la biashara zao.
Kupitia program hii ya Imarika, Her Initiative inaamini kwamba wasichana wajasiariamali watapata nafasi ya kuku ana kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii hasa kufuatia kufuatia athari zilizotokana na mlipuko wa janga la corona.
Social Plugin