Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA : WATANZANIA TUMCHAGUE DKT MAGUFULI NI KIONGOZI MAKINI


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kumchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa sababu ni kiongozi makini, shupavu, mbunifu na mwenye uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wote.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake, Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na yamewanufaisha Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Septemba 8, 2020) alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Matadi kata ya Ndemet wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.

Amesema Watanzania wanatakiwa wamchague Rais Dkt. Magufuli ili aweze kuwaongoza katika kusimamia vizuri matumizi ya rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini. Amesema Tanzania ni nchi tajiri yenye uwezo wa kuwaletea wananchi wake maendeleo bila ya utegemezi, hivyo wachague viongozi makini kwa manufaa ya Taifa.

“WanaSiha wote nimekuja hapa kwenu leo nina kazi moja tu ya kumuombea kura mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, Rais Dkt. Magufuli ambaye ni kiongozi imara, mzalendo na mchapakazi, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Mollel na wagombea udiwani wote wa CCM katika wilaya hii. Ikifika siku ya kupiga kura tuhakikishe tunawachagua.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa lazima wananchi waamini kwamba uongozi unatoka kwa Mwenyezi Mungu na Rais Dkt. Magufuli ameletwa na Mwenyezi Mungu, hivyo amewaomba wampe ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano mingine ili aendeleze kazi za maendeleo alizozianza.

“Nawasihi inapofika siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu tunapotumia haki ya msingi ya kidemokrasia, tukamchague Rais Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi anayejali maslahi ya Watanzania wote na ni kiongozi anayeweza kujua nchi inawakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara ambao kila mmoja anatakiwa afanye shughuli zake kwa uhuru bila ya kusumbuliwa.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa Siha kuwa Serikali itayarudisha mashamba yote ya Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) yanayomilikiwa kinyemela na watu wachache kwa manufaa yao binafsi

“Kuna watu wamejimilikisha mahekari ya mashamba ya KNCU ambayo ni mali zenu, nawahakikishia tutawanyang’anya na kuyarudisha kwenu ili atakayelima alime, atakayefuga afuge”

Amesema KNCU ni mali ya wananchi (wanaushirika) na kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ya kurudisha hadhi ya ushirika katika kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani waliohusika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo na itaendelea kurejesha mali zote kwa wananchi ili wafanyie shughuli za maendeleo.

Akizungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Siha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 60 vilivyopo Siha vijiji vyenye umeme ni 58 na viwili tu ndio havina umeme na kwamba navyo vitaunganishwa umeme, amewaomba wakazi wake waendelee kuwa na subira.

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.


 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com