WATOA HUDUMA MITANDAONI WATAKIWA KUWAHIMIZA WANANCHI KUZINGATIA SHERIA ZA UCHAGUZI


Na Jovina Bujulu, MAELEZO Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera ametoa wito kwa watoa huduma za habari mitandaoni (online media), kuwasisitiza na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume katika kipindi hiki ambapo Taifa liko katika kampeni za uchaguzi kuelekea katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 28, 2020 ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu.


Aidha, amewashukuru kwa kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake na kuiwezesha kuwa karibu na wadau wa uchaguzi kwa njia ya taarifa na kutoa habari kwa wakati na kuiwezesha Tume kutumia mitandao kwa kutoa ya elimu ya mpiga kura pamoja na kufafanua hoja mbalimbali kutoka kwa wadau.


“Ipo mitandao ambayo imetoa nafasi ya kuchapisha, kutangaza habari, na makala za kuelimisha umma kuhusu Tume na majukumu yake, kupitia redio na runinga za mitandaoni, tume imeshiriki vipindi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu kwa wapiga kura”, amesema Dkt. Mahera.


Kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi katika taifa lolote duniani ni hatua muhimu ambapo wananchi wanatakiwa kuwa wamoja na kuonesha mshikamano ili kuepuka vurugu na fujo zisizo na tija ambazo zinaweza kuchochewa na vyombo vya habari, iwe ni magazeti, runinga au mitandao ya kijamii kwa kuchapisha au kutangaza habari zenye viashiria vya uchochezi.


Hiki ni kipindi kinachokuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa, hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. Katika kipindi hiki vyombo vya habari vinapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha haviwi chanzo cha joto hilo kwa kuzingatia misingi na maadili ya kazi zao.


Dhamana ya vyombo vya habari katika kipindi hiki ni kuhakikisha vinajiepusha kutumiwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kwa kujikita katika majukumu yao ya msingi ambayo ni kuhabarisha na kuliemisha wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii. 


Hivyo, ni jukumu la vyombo hivi kuwa na umakini mkubwa sana ili kuhakikisha vinawatendea haki wananchi wake kwa kuwapasha habari wanazotakiwa kuzisikia na kuzisoma ikiwa ni pamoja na maendeleo yaliyofanywa na viongozi wao na wanayotarajia kuyafanya  pamoja na na kuwapa nafasi wagombea uongozi kunadi sera na Ilani za vyama vyao.


Dkt. Mahera amesema Tume inawatambua watoa huduma za mitandao kwa kuwa wanatumika kama daraja linalounganisha Tume na wadau kwa njia ya mawasiliano na pia kama mojawapo wa wadau muhimu wa uchaguzi wenye dhamana ya kuhabarisha wananchi.


Dkt. Mahera amesema hayo wakati wa kikao kati NEC na watoa huduma ya habari wakiwemo ‘Blogers’ pamoja na runinga (TV) na redio za mtandaoni kutoka maeneo mbalimbali nchini kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar-es-Salaam. 


“Tume inaamini kuwa mkipata uelewa mzuri wa michakato ya uchaguzi, basi itakuwa rahisi kwenu kuwaelimisha na kuwahabarisha wananchi kupitia vyombo vyenu vya habari ili kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020”, amesema Dkt. Mahera.


Kutokana na kukua kwa teknolojia, vyombo vya habari vya mitandao vimekuwa vikitoa habari kwa uharaka zaidi kuliko vyombo vya habari vilivyozoeleka kwa jamii hasa magazeti ambayo habari zake huwa zinasomwa siku inayofuata. Hivyo, mabadiliko hayo wakati mwingine yanawafanya vyombo vya habari vya mitandao kukosa umakini na wakati mwingine kuandika habari zenye kupotosha jamii.


Kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, watoa huduma ya habari za mtandao wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa kuwahamasisha wananchi hasa wapiga kura kushiriki katika kampeni ili waweze kuwapima sera za wagombea na hatimaye kujitokeza kwa wingi kupiga kura.


Ili kuhakikisha wanaandika, kuchapisha au kutangaza habari zenye ulinganifu, watoa huduma ya habari mtandaoni wanatakiwa kutoa kipaumbele kwa masuala yanayoelekea kujenga umoja wa kitaifa badala ya kutoa habari zinazochochea vurugu huku wakizingatia kuwa Tanzania sio kisiwa na kwamba wasipotumia vizuri taaluma yao wanaweza kuingiza nchi kwenye machafuko kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi.


Vyombo vya habari, vinatakiwa kuwa na uvumilivu wanapotafuta habari kuhusu uchaguzi kwa kutafuta ufafanuzi kutoka katika chombo kinachohusika ambacho ni Tume ya Taifa ua Uchaguzi (NEC), ambacho kimeahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha pale watakapohitaji ili kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.


Kwa upande wake, Kamishna wa NEC, Asina Omari aliwakumbusha watoa habari hao kuwa vyombo vyao ni muhimu kwa wapiga kura na kuwasisitiza wao wenyewe pia wazingatie majukumu yao ya msingi.


Fauka ya hayo, amewataka watoe elimu ya uchaguzi kufuatana na muktadha wa vyombo vyao, kutoa habari kutoka kwenye vyanzo sahihi na wawe na taarifa sahihi kabla hawajachapisha au kutangaza jambo lolote kuhusu mchakato mzima kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi hata baada ya uchaguzi ili sote tubaki tukiwa Watanzania.


Naye Mkurugenzi Msaidizi Habari na Elimu ya Mpiga Kura kutoka NEC, Dkt. Cosmas Mwaisobwa amewahimiza watoa huduma hao watambue wajibu wao wa kuchapisha na kutangaza habari za mchakato wa uchaguzi, mahali pa kupigia kura, haki na wajibu wa mpiga kura ni masuala muhimu ya kuwaelimisha wananchi kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura na hatimaye kupata viongozi bora nchini.


Aidha, amevitaka vyombo hivyo kuwa na uelewa juu ya mamlaka na majukumu ya NEC ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Tume Kikatiba, uteuzi wa viongozi wa Tume na utofauti wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaosimamiwa na TAMISEMI na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge  na Madiwani pamoja na kuwa na  ufahamu kuhusu Sheria za Uchaguzi na matakwa yake.


Dkt. Mahera amesema kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lina jumla ya wapiga kura 29,188,347 na vituo vya kupiga kura 80,155 ambapo kila kituo kitakuwa na wapiga kura wasiozidi 500.


MWISHO




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post