Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kagera
Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayolima na kuzalisha kwa wingi zao la Kahawa hapa nchini ambapo imeelezwa kuwa pamoja na uzalishaji huo wananchi wa mkoa huo hawana utamaduni wa kunywa kahawa wanayoilima wao.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo jana Tarehe 4 Septemba 2020 alipofanya ziara katika kiwanda cha kahawa cha AMIMZA kilichopo halmashauri ya wilaya Bukoba Mkoani humo ambapo amesema kuwa wananchi wa mkoa huo ni wakulima wazuri wa kahawa ila sio watumiaji wa kahawa yao.
“Wananchi wa Bukoba pamoja na watanzania kwa ujumla wake kama wangeweza kutumia ipasavyo kahawa yao tusingekuwa na tatizo la masoko ya kahawa, hivyo nawasihi wananchi wenzangu kuhakikisha kuwa mnatumia kahawa ipasavyo ili kuimarisha soko letu la ndani” Amesema Waziri Hasunga
Hasunga ameongeza kuwa Kahawa inayolimwa Kagera imekuwa Kahawa bora Duniani ambayo hupelekea baadhi ya makampuni huko ulimwenguni kuitumia kwa kuiwekea Lebo nyingine ambao hunufaika Zaidi na kahawa yetu kutokana na faida zilizopo kwenye zao hilo.
“Watanzania hasa wanakagera hawana utamaduni wa kunywa kahawa pamoja ya kuwa sisi wenyewe ni wazalishaji wa kubwa wa Kahawa hapa nchini, naona ipo haja ya watu wetu kuelimishwa faida za unywaji wa kahawa. Lakini nawapongeza sana kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya hapa Kagera.” Amesema Waziri Hasunga
Ameongeza kuwa mkoa wa Kagera unayo fursa nyingi za uwekezaji hasa za viwanda na kuwasihi wawekezaji kujitokeza kwa kuwa usalama ni wa kutosha na kuongeza kuwa zao la kahawa linatakiwa kuwa zao bora nchini kama watanzania wataamua kulipa umuhimu na nafasi.
Kwa niaba ya mmiliki wa kiwanda cha AMIMZA Ndg Billal Amir Hamza amesema kuwa amesema kuwa kiwanda hicho kipo katika maboresho kwa kuongezea baadhi ya idara na kuongeza kuwa kikikamilika kitaweza kutoa ajira kwa watanzania Zaidi ya 600.
Billal ameongeza kuwa kiwanda kikikamilika kitaweza kuzalisha kahawa mumunyifu (Instant) tani 6,000 sawa na tani 18,000 za kahawa safi ambazo ni sawa na tani 36,000 za kahawa ya maganda ambayo ni mara mbili kutokana na gredi ya kahawa.
“Mpaka sasa pamoja na uzalishaji unaoendelea tumeajiri wafanyakazi 59 pamoja na kutoa ajira nyingine kwa wananchi ambao ni majirani zetu hapa ambapo pia tumejenga kiwanda kikubwa Africa Mashariki na kati, niseme tu sisi soko letu lipo nje ya nchi ila kwasasa tumerudi nyuma baada ya janga hili la Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona baada ya baadhi ya nchi kufunga mipaka yake.” Amesema Billal
MWISHO
Social Plugin