WAZIRI WA KILIMO AZINDUA MATREKTA 7 NA ZANA ZAKE ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU NA MICHE BORA YA MAZAO


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Katika mwaka 2019/2020, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) katika fedha zake za maendeleo pamoja na mambo mengine ilitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya mashamba ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora kwa lengo la kuchangia upatikanaji wa mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya Wakala wa Mbegu (ASA),  Makampuni binafsi yanayohitaji mbegu za awali kutoka TARI, na hatimaye kusambazwa kwa wakulima.



Mwaka 2019/2020, Serikali imetoa fedha za kuweza kununua matrekta saba (7) na zana zake ambazo zitatumika katika kupanua mashamba ya uzalishaji wa mbegu na miche bora ya mazao na pia kuimarisha mashamba ya utafiti kwa kuzalisha aina mpya za mbegu bora za mazao mbalimbali.

Wizara ya Kilimo, kupitia ASDP II imeendelea kuimarisha mazao ya Kimkakati ikiwa ni pamoja na Michikichi, Korosho, Pamba, Ngano, Mkonge, Alizeti, Mahindi, Mtama, Uwele na Zabibu. Aidha, Mikakati hii ya Wizara chini ya ASDP II imechagiwa zaidi  na msisitizo wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassimu Majaliwa Majaliwa ambaye amehamasisha uzalishaji wa kilimo cha Michikichi na Mkonge hapa nchini. Katika uhamasishaji huo, Wizara kupitia TARI imeweza kuzalisha miche milioni 2 kwa mwaka 2019/2020 na inategemea kufikia miche milioni 41 mwaka 2025.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 1 Septemba 2020 katika eneo la Makutupora Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Matrekta na zana zake ili kuimarisha uzalishaji wa mbegu unaofanywa na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) na kuongeza kuwa hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali zitakidhi mahitaji ya mbegu nchini.

Amesema kuwa Matreka hayo yaliyozinduliwa yamelengwa kuongeza uwezo wa TARI katika kuzalisha mbegu bora kutoka takribani tani 1,000 kwa sasa hadi kufikia tani 10,000 mwaka 2025. Vile vile, katika kipindi hicho, TARI itaweza kuzalisha miche kutoka milioni 10.3 ya sasa hadi kufikia miche milioni 40 mwaka 2025.

Waziri Hasunga amesema kuwa upatikanaji wa matrekta hayo utaimarisha upatikanaji wa mbegu mbalimbali ikiwemo mbegu za Michikichi zitakazoiwezesha serikali kuwa na utoshelevu wa mafuta ya kula.

Ameongeza kuwa ili kuwe na usalama wa chakula ni lazima msisitizo mkubwa uwekwe kwenye usimamizi madhubuti kwenye sekta ya mbegu ili kuwe na mbegu bora za kutosha na zenye bei nafuu kwa wananchi.

Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali imekusudia kuongeza uzalishaji wa mbegu mbalimbali za nafaka, Mboga na matunda kadhalika mazao ya mafuta

Hasunga amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kuhakiisha inaongeza juhudi za kuchakata mazao yatokanayo na kilimo ili kuongeza thamani ya mazao na hatimaye kuimarisha upatikanaji wa malighafi za viwandani.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post