Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amezindua zoezi muhimu la ugawaji wa mbolea bure kwa wakulima wa Mkoa wa Songwe ili waweze kuitumia katika msimu wa kilimo 2020/2021.
Amesema kuwa mkoa wa Songwe umekuwa ukizalisha chakula kwa kiasi kikubwa huku ukishika nafasi ya tatu kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya Nafaka baada ya Ruvuma na Rukwa.
Pia amewapongeza Wanasongwe kwa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wa kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza tija kwenye mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya mbolea.
Hasunga amesema kuwa msaada huo wa kampuni ya YARA ni chachu kubwa ya kuendelea kuzalisha kwa wingi zaidi ili kujihakikishia usalama wa chakula na pia kurahisisha uwezo wa kuuza chakula mdani na nje ya nchi.
Ameataka watanzania kutembea kifua mbele kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawajali watanzania wote.
Hasunga ameeleza kuwa, Nchi nyingi za jirani zinaitegemea Tanzania kwa chakula kwa hivyo mbolea hiyo iliyotolewa kwa wakulima itasaidia kuzalisha zaidi na kuuza zaidi katika nchi hizo.
"Hii itawaongezea kipato lakini Serikali pia itakusanya kodi nyingi zaidi kutokana na mauzo ya mazao haya ili kuweza kutekeleza miradi zaidi ya maendeleo" Amesisitiza Waziri Hasunga
Msaada huo una thamani ya Bilioni 16.5 wenye uzito wa MT12,500 hivyo Waziri Hasunga ametoa mwito kwa wakulima kuitumia vyema mbolea hiyo ili waweze kuwa na matokeo makubwa yatakayoongeza tija na Pato la Taifa.
Pamoja na mbolea hio ya bure, wakulima pia watapata ushauri wa bure kutoka YARA kuhusu namna ya kutumia mbinu za kisasa za kidijitali za kuongeza uzalishaji ili kuhakikisha Mkoa wa Songwe unazalisha chakula cha kutosha, ili wakulima waweze kujiongezea kipato na pia kuhakikisha afya bora kupitia uzalishaji wa vyakula vyenye rutuba sahihi.
Hasunga amewataka wakulima kupitia vyama vya msingi kuhakikisha msaada huo unatumika vizuri ili matokeo yake yawe mazuri na kwa wakati. "Tusisite kuomba ushauri kutoka YARA pale ambapo tunakwama, kwani wamejitolea kutoa ushauri wa kitaalamu bure jambo amabalo ni muhimu sana na la kuigwa" Amesema Waziri Hasunga
MWISHO