Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ameiteua Benki ya CRDB kuwa balozi wa mazingira wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Pendezesha Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya Goba, iliyopo Dar es salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, Waziri Zungu aliipongeza Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa mikakati ya kusaidia jitihada
za Serikali katika kutunza na kuboresha mazingira kupitia kampeni hiyo yaPendezesha Tanzania ambayo inahamasisha umuhimu wa upandaji miti katika kutunza mazingira.
Waziri Zungu amesema kampeni ya Pendezesha Tanzania imekuja wakati muafaka kwani inaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kupanda miti Milioni Moja na Laki Tano kwa kila Halmashauri kwa mwaka ili kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.
“Niipongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuwahamasisha watanzania kutunza mazingira yao yaliyowazunguuka. Niwaahidi Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuboresha na kuyatunza
mazingira yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri Zungu huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano Benki ya CRDB katika kuweka kipaumbele suala la utunzaji wa mazingira.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuzindua kampeni ya Pendezesha Tanzania katika mkoa wa Dar es Salaam.
Kunenge aliwataka wananchi wa mkoa huo kupanda mti mmoja kila mtukatika makazi yao kama sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo.
“Asanteni sana Benki ya CRDB kwa kutupa heshima wakazi wa Dar es Salaam ya kutupendezeshea jiji letu. Niwaahidi kuwa tutashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema
Kunenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya benki hiyo kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida kila
mwaka kusaidia nyanja za elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
“Lengo la kuzindua kampeni hii ni kuendelea kuihamasisha jamii kuona jukumu la kupanda miti ni la jamii nzima. Tumeanza kwa kupanda miti 2000 katika shule zote za msingi na za sekondari zilizo katika Kata ya Goba kwa lengo la kuzifanya shule
hizi kuwa na mazingira bora na rafiki kwa watoto kusoma,” alisema Nsekela
Kampeni ya Pendezesha Tanzania inatarajiwa kufanyika nchi nzima ili kusaidia kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupanda na kutunza miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeanza Dar es Salaam katika shule hizi zilizopo
katika kata ya Goba, lakini lengo letu ni kufika katika wilaya na vijiji vyote Tanzania,” aliongezea Nsekela.
Sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania, Benki ya CRDB pia imetoa msaada wa pampu za maji kwa shule za Sekondari za Fahari, Goba na Kinzudi ili kusaidia kuboresha upatikanaji wa maji katika shule hizo.
Akizungumza juu mikakati ya biashara inayozingatia mazingira, Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea mfumo wa biashara ambao unazingatia utunzaji wa mazingira ikiwamo kuweka sera inayoelekeza utoaji wa mikopo kwa miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira, kuanzisha huduma na bidhaa za kidijitali, pamoja na kuwekeza katika mifumo ya ufanyaji kazi inayopunguza matumizi ya karatasi.
Afisa elimu kata ya Goba, Edward Shilamba aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti katika shule za Sekondari na Msingi kata ya Goba. Afisa elimu huyo alimhakikishia Waziri wa Mazingira kuwa wataweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha miti hiyo inastawi kama inavyotarajiwa.
Kutokana na jitihada za kusaidia utunzaji mazingira mpaka, mwaka 2019 Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuweza kutambuliwa na kupata usahili katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshugulikia
masuala ya Tabia Nchi “United Nations Green Climate Fund (GCF)”.
Kupitia usahili huu, Benki ya CRDB sasa inaweza kushiriki katika kuwezesha miradi mikubwa ambayo ni rafiki wa mazingira, kwa kutoa mikopo ya hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.