Meneja wa Mradi wa ENRICH, Bi Mwivano Malimbwi (aliyesimama) akitoa mafunzo maalum ya malengo ya mradi huo ya utoaji wa elimu ya lishe na kuboresha afya ya uzazi kwa vijana balehe kwenye mikoa ya Singida na Shinyanga kwa waandishi wa habari ya Mkoa wa Singida (hawapo pichani) leo, aliyekaa ni mtaalam wa Jinsia na Utetezi wa Mradi huo Tumaini Fred
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akiangalia mazao ya asali na mashine ya kukamulia asali ya kikundi cha ufugaji wa nyuki mkoani Singida kinachofadhiliwa wa World Vision
**
Na. John Mapepele,Singida
Shirika la World Vision nchini limewataka waandishi wa habari kama wadau wakuu wa Shirika hilo kutoa taarifa sahihi za kazi za shirika hilo kwenye mradi wake wa ENRICH ambao unatekelezwa katika mikoa ya Singida na Shinyanga.
Mradi huo unalengo la kupeleka elimu ya lishe na afya ya uzazi kwa vijana balehe vijijini ili kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto chini ya siku 1000 na ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ili kuboresha maisha ya watanzania.
Akitoa mafunzo maalum kuhusu malengo wa mradi kwa waandishi wa Mkoa wa Singida , Meneja wa Mradi wa ENRICH Bi, Mwivano Malimbwi amesema mradi huu ni wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2021 na umejikita katika kuwezesha huduma za lishe ili kuimarisha afya ya mama na mtoto kwa gharama za dola milioni 8.4 za Canada.
Kwa mujibu wa Malimbwi malengo mahususi ya ENRICH ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa kuangalia visababishi vya vifo hivyo ambapo mradi umeelekeza nguvu kwenye kuimarisha mifumo ya utoaji wa afya katika vituo vya kutolea huduma hizo.
Aliongeza kuwa awali wakati mradi ulipoanza walibaini changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kumchunguza hali ya kiliishe ya mtoto vilikuwa na upungufu mkubwa ambapo vituo vichache vilikuwa na vifaa hivyo vya kupimia urefu na mzingo wa kati wa mkono kwa akina mama na mtoto.
Alisema watoa huduma wachache walipata mafunzo ya afya ya lishe kwenye ngazi ya mkoa na wilaya ambapo hakukuwa na watoa huduma katika maeneo ya vijijini.
Aidha alisema pia hakukuwa na elimu ya uongozi kwenye kamati za afya za mikoa na wilaya ambapo Mradi uliwajengea uwezo ili kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa pamoja badala ya kuwa watoa maamuzi.
Aidha mipango na bajeti ilikuwa ikifanywa kwa hisia badala ya kutumia takwimu sahihi.
Malimbi amesema lengo la pili la Mradi ni kuongeza uzalishaji wa chakula chenye uwingi wa virutubisho ambapa kwenye eneo hili amessisitiza kuwa mkakati umekuwa katika kuongeza uzalishaji ulioongezwa kibailojia, kuongeza utumiaji wa virutubishi kwa watoto na sayansi ya ulaji na ufyonzaji wa virutubishi.
Alisema pia katika mikoa ya Singida na Shinyanga imebarikiwa kuwa na vyakula vya makundi yote na matunda ya asili kama sasati, rade na furu ambayo kama yakitumika kikamilifu yatasaidia sana kuboresha lishe na kupunguza udumavu kwa watoto.
Alipongeza jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dk. Rehema Nchimbi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa suala la lishe na afya ya uzazi vinakuwa kipaombele cha kwanza kwa wananchi ambapo pia amesema amehamasisha ulaji na ulimaji wa viazi lishe na kuwafanya wananchi wa Mkoa wa Singida tofauti na awali ambapo vilikuwa vikiuzwa nje ya Mkoa.
Aidha amesema Mradi umehamasisha akina mama kulima bustani za mbogamboga kwenye kila kaya ili kuhakikisha kuwa kwenye kila mlo mboga zinakuwepo.
Amesema lengo la mwisho la mradi huo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwajibikaji wa wadau wote muhimu na kila mmoja anafanya majukumu yake kwa ufasaha, ambapo ametolea mfano kuwa Serikali kama mdau mkuu ina wajibu wa kuweka vituo vya kutolea huduma na mtoa huduma ambapo jamii inawajibu wa kuvitumia vituo hivyo na watoa huduma.
Mradi wa ENRICH ni Mradi wenye sekta nyingi na unafadhiliwa na Serikali ya nchi ya Canada ambapo unatekelezwa kwa kushirikiana na wabia ambao ni Nutritional International, Canadian Society for International Health anayejikita katika kuimarisha mfumo wa afya.
Ikiwemo Harvest Plus, kwenye Sekta ya Kilimo, Chuo kikuu cha Toronto katika kufanya tathimini na ufuatiliaji wa mradi na World Vision ambaye ni msimamizi mkuu wa fedha wa mradi huo. Serikali ya Tanzania ni mtekelezaji namba moja chini ya TAMISEMI.