Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka akinadi wagombea wa CCM,Kushoto ni aliyekuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo, Kulia ni mgombea udiwani kata ya Bumera-Tarime, Deogratius Ndege.
Na Dinna Maningo, Tarime
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka na baadhi ya wagombea udiwani wamemuombea kura mgombea udiwani kata ya Bumera-Tarime, Deogratius Ndege na kuwaomba wananchi wamchague kwakuwa ni mtu wa vitendo.
Wakizungumza leo Jumatatu Oktoba 5,2020 wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea huyo ambaye amekuwa Diwani kwa miaka mitano iliyopita , Airo aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi alisema kuwa sababu ya kushiriki kwenye uzinduzi wa kampeni zake ni kutokana na ushiriki wake katika udhibiti wa wizi wa ng'ombe uliokuwa tishio katika kata hiyo na majirani zao wa Rorya.
"Tumeshirikiana sana na Ndege kudhibiti wizi wa mifugo ni mtu ambaye amekuwa akichukiwa na baadhi ya wananchi kisa kuwafatilia wezi kuhakikisha wanakamatwa,hakuogopa sasa watu wanalala usingizi,wizi uliopo ni wa ng'ombe moja au wawili tena kwa mara chache na kuna wakati wakiiba wanapatikana.
"Ndege amejitahidi kuleta maendeleo kwenye kata yake zaidi ya shilingi bilioni moja zimetekeleza miradi mbalimbali na hii inatokana na ufuatiliaji wake wa karibu kuhakikisha anapata fedha za miradi. Kuna wengine wakishakuwa viongozi hawarudi kwenye kata zao akishachukua mkopo humuoni tena anashindwa kujua matatizo ya kata yake", alisema Airo.
Alisema kuwa wizi unarudisha nyuma maendeleo, hivyo kuwaomba wananchi kuachana na kazi hiyo na kutafuta kazi halali za kuwaingizia kipato pamoja na kujishughulisha na kilimo kwa kuwa wizi unahatarisha usalama na amani ya wananchi na kwamba ni vyema kukemea wale wanaovuruga amani.
Katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka alisema kuwa Ndege ni miongoni mwa Madiwani wa CCM waliofanya maendeleo kwenye kata zao walipokuwa madiwani licha ya halmashauri ya wilaya ya Tarime kuongozwa na CHADEMA,lakini alijenga hoja na kueleza kero mbalimbali za kata yake ambazo nyingi zilitatuliwa ikiwemo utekelezaji wa miradi.
"Shida ya CHADEMA,Serikali ya CCM ikifanya maendeleo wanasema ni kwa sababu yao lakini yale ambayo hayajafaywa wanasema ni CCM kama umeme haupo wanasema Serikali haijaleta umeme lakini umeme ukiwepo wanasema umeletwa na wao.
"Ndege alikuwa anasimamia maendeleo mkimpa kura na mkampa ubunge Waitara maendeleo yatazidi,eti wanasema kwamba Ndege kaiba fedha sasa aliwezaje kuiba fedha na wakati halmashauri inaongozwa na Chadema,Mwenyekiti wa halmashauri ni wa Chadema na Mbunge ni mjumbe kwenye vikao sasa Ndege mtu mdogo anawaibiaje pesa halafu mnalalamika bila kuwa na ukweli wowote"alisema MKaruka.
Mgombea udiwani Deogratius Ngede alieleza yaliyofanyika wakati wa udiwani wake kwamba kwa miaka mitano 2015-2020 kata yake imepokea fedha kutoka Serikalini zaidi ya shilingi Bilioni moja zilizotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na michango ya wananchi.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Daraja la mto Mori Kitenga-Kiterere iliyogharimu milioni 525,Barabara ya Kitenga-Kiterere milioni 31,Barabara ya Buguta-Mang'ore milioni 15,Barabara ya Kitenga-Nseko milioni 21 ambayo bado ujenzi wake unaendelea.
Miradi mingine ni Karavati lililojengwa mto Kurusiaga milioni 35 ujenzi unaendelea,Daraja la mto Mirare kwenda Mantamamkwe milioni 45,kulima barabara mita 500 ya Changuge na kutoa mawe iliyogharimu milioni 3.5 jumla ya miradi yote ya miundombinu ni sh 725,500,000.
Akizungumzia upande wa Afya Ndege alisema miradi iliyotekelezwa ni ukarabati wa Zahanati ya Kitenga sh.milioni 42,ukarabati RCH Kitenga sh.milioni 15,ambapo fedha ziko kwenye akaunti ya kijiji,Zahanati ya Turugeti imetengewa fedha 9,800,000 ipo kwenye Akaunti,Zahanati ya Kiterere imetengewa fedha milioni 15 fedha bado ipo Serikali kuu.
Katika Elimu alisema kuwa shilingi milioni 6 zimekamilisha chumba kimoja cha darasa shule ya msingi Kitenga na choo cha walimu sh milioni 5, kukamilisha chumba kimoja cha darasa na ofisi ya mwalimu mkuu shule ya msingi Kwisarara iliyogharimu milioni 6 na ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa sh.laki 9.
Ujenzi wa darasa moja shilingi milioni 6,choo cha muda sh laki 9 shule ya msingi Turugeti,ujenzi wa choo cha kisiasa kwenye shule hiyo utakaogharimu milioni 12 kazi inaendelea.Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa sh 12,000,000,choo cha waalimu milioni 5,michango ya wananchi milioni 8 iliyofanikisha kujenga choo cha kisasa.
Miradi mingine ni ujenzi wa madarasa 4 na ofisi ya za waalimu shule ya msingi Taisi milioni 18,Choo cha kisasa shilingi milioni 10,milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya waalimu pesa zipo kwenye akaunti ya shule.
Ndege akizungumzia suala la madawati alisema kuwa kata hiyo imepata madawati 225 jumla ya fedha sh.milioni 11,250,000,ukamilishaji wa jengo la utawala kwa awamu ya kwanza milioni 20.
"Tulipata ufadhili kwa aliyekuwa mbunge wa Rorya Lameck Airo alitupatia mifuko 100 ya Saruji yenye jumla ya milioni 2 na kuisambaza kwenye vijiji vyote vinne,alitupatia mabati 34 yenye thamani ya sh. 850,000,Steven Mathayo alitupatia mabati 24 ya laki 6 yapo kijiji cha Kitenga,jumla ya miradi ya elimu tumepokea milioni 117,300,000/=.
Ndege alisema kuwa katika huduma ya maji wamejenga kisima kifupi cha maji kijiji cha Kwisarara kwa milioni 20,ujenzi wa visima vifupi viwili kijiji cha Kiterere milioni 45,kisima kirefu kijiji cha Kwisarara sh.milioni 15 kitakachosambaza maji kata ya Bumera.
Alisema kuwa umeme wa Rea umesambazwa katika vijiji viwili kati ya vinne ambavyo ni Kwisarara na Turugeti,kuhusu kilimo wameanzisha shamba darasa kilimo cha mihogo na shamba darasa kilimo cha migomba.
"Kwenye vikao vya madiwani nilikuwa najenga hoja nawasumbua sana halmashauri kuhusu miradi licha yakwamba halmashauri kuongozwa na Chadema sikusita kufatilia mpaka kuna wakati nilitolewa nje ya vikao ni kwasababu ya kuwabana na kujenga hoja mbalimbali nawashukuru wananchi kwa kuniamini na kunituma niwawakilishe naombeni kura tena nimalizie yaliyosalia"alisema Ndege.
Alisema kuwa miradi yote imetekelezwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli na yeye kama Diwani mwakilishi wa wananchi nakwamba endapo wananchi watamchagua wataanzisha shule mpya ya Runyerere kijiji cha Turugeti,mradi wa maji wa kisima kirefu kijiji cha Turugeti na kusambazwa katika vijiji vyote.
"Kuzifungua Zahanati ili zianze kazi,kujenga nyumba ya Madaktari Zahanati zote kata ya Bumera,kujenga barabara Runyerere-Kikomori,Kujenga barabara Bunyama-Bukiro-Taisi,kujenga kituo cha Afya cha Kata,kujenga Hosteli ya wasichana shule ya Sekondari Kurumwa" alisema.
Aliongeza kuwa kitajengwa chuo cha ufundi Kigomba Taisi,ujenzi barabara ya Kiterere,barabara ya Buguta-Nyerema-Kiterere Rodi,ujenzi wa majosho ya kuogeshea mifugo,kuanzisha kilimo cha zao la mkonge,migomba,Alizeti,mikopo ya riba nafuu kwa vijana,na walemavu,kuimarisha ulinzi na usalama,ujenzi wa shule mpya ya Mwita na kukomesha wizi wa mifugo.
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo, akimnadi mgombea udiwani kata ya Bumera-Tarime, Deogratius Ndege (kulia).
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo, akimnadi mgombea udiwani kata ya Bumera-Tarime, Deogratius Ndege (kulia).
Lameck Airo akimzawadia Msanii wa ngoma za asili
Pendo akipiga magoti kumuombea kura Mme wake Deogratius Ndege
Lameck Airo akiteta jambo na katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka