Askofu Liberatus Sangu
Na Simeo Makoba - Simiyu
Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amewataka Wakatoliki na Watanzania wote kuepuka kuwa chimbuko la machafuko katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
Askofu Sangu ametoa rai hiyo leo Jumapili Oktoba 25,2020 katika misa ya Kipaimara iliyofanyika katika Parokia ya Mwanhuzi wilayani Meatu moani Simiyu zikiwa zimebaiki siku mbili tu za kufanyika kwa zoezi la upigaji wa kura kumchagua Rais,Wabunge na Madiwani.
Askofu Sangu amewataka Watanzania kujitokeza kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka huku wakizingatia maelekezo yanayotolewa na Mamlaka zilizowekwa pamoja na kuhakikisha hawashiriki matukio ya aina yoyote ambayo yanahatarisha amani ya nchi.
“Mkatoliki yeyote mahali popote ulipo usiwe chimbuko la machafuko, timiza wajibu wako wa kupiga kura na kurudi nyumbani, mengine yote ya kuleta vurugu yanatoka kwa muovu na mwenye pepo , tujitayarishe sote kupiga kura kwa amani tukiongozwa na Mungu roho mtakatifu”, amesema Askofu Sangu.
Askofu Sangu amebainisha kuwa amani iliyopo nchini ni tunu pekee ambayo Tanzania imetunukiwa na kwamba kila mmoja anapaswa kuhakikisha anailinda ili iendelee kuwepo.
Katika hatua nyingine Askofu Sangu amewataka watu wote kuwa wajumbe wa amani na ametoa maelekezo kwa waamini wa jimbo lake kusali sala maalum ili kuombea amani ya nchi katika kipindi hiki taifa linapoelekea katika kipindi maalum cha uchaguzi.