Imeelezwa kuwa Ofisi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara zilizopo Mjini Shinyanga imenusurika kuchomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Jumapili Oktoba 25,2020.
Taarifa ya Ofisi ya CHADEMA kunusurika kuchomwa imetolewa na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami leo Jumapili Oktoba 25,2020 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Shinyanga.
“Leo majira ya saa saba usiku ofisi yetu ya Kanda ya Serengeti imenusurika shambulio la kuchomwa moto. Tulipewa taarifa na walinzi wetu kwamba kioo cha dirisha la ofisi ya Katibu kimevunjwa,na baadaye tumejaribu kuangalia labda ni vibaka walitaka kuiba lakini tulivyoingia ndani tukakutana na hali ambayo inaonesha kulikuwa na watu wenye nia ovu ya kulipua kwa petroli. Tumekuta chupa yenye mafuta ya petroli kiasi cha lita moja na nusu na utambi ndani na ukiwa umeunguzwa kidogo ikionesha kwamba huyo mtu alikuwa amewasha moto na bahati nzuri moto huo haukuwaka”,ameeleza Mnyawami.
Aidha Mnyawami amelishukuru Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha na kwamba wameliachia jeshi la polisi kuendelea na upelelezi kuhusu tukio hilo.
“Kwa kweli kwa tukio hili la uchomaji Tunalishukuru sana jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano wa kutosha waliotupatia. Mtu wa kwanza kufika hapa baada ya sisi kutoa taarifa polisi ni OCD pamoja na askari wake , tunawashukuru sana. Lakini pia nimshukuru Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Shinyanga amefika eneo la tukio kujionea hali halisi. Polisi wametoa ushirikiano mzuri na mambo mengine ya Kiupelelezi tumewaachia wao”,amesema Mnyawami.
Aidha amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda Kupiga Kura Oktoba 28,2020 kuchagua viongozi wanaowataka.