Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WOWAP YATOA ELIMU YA MPIGA KURA MKOANI SINGIDA

Mratibu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Women Wake-up (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mtamaha wakati akitoa elimu ya uraia ya mpiga kura katika Manispaa ya Singida juzi.
Wananchi wa Kijiji cha Mtamaha wakiwa kwenye mkutano wa kupatiwa elimu hiyo ya mpiga kura.
Mmoja wa Wananchi akiuliza swali kuhusu elimu ya uraia ya mpiga kura.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika hilo, Issah Shayo akitoa elimu ya uraia ya mpiga kura kwa waendesha bajaj,

Na Waandishi Wetu, Singida.

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) kwa wiki mbili mfululizo limeendelea kusambaza elimu ya uraia ya Mpiga Kura kwa wananchi wote wa mkoa wa Singida na vitongoji vyake, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwana-Singida anatumia haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi sahihi kuelekea uchaguzi mkuu.

Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka WOWAP, Issah  Shayo alisema azma hasa ya mafunzo hayo ni kuelimisha na kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao muhimu wa kuhakikisha wanachagua viongozi bora kwa maendeleo yao katika muktadha wa kauli mbiu isemayo ‘Kura yako, Sauti yako’

“Tunawasihi wananchi wote wa Singida, ifikapo Oktoba 28 twendeni tukapige kura ili kupata viongozi watakaoamua mustakabali wa maisha yetu na vizazi vyetu…kumbukeni kura yako ndiyo sauti yako,” alisema Shayo.

Alisema shabaha ya mafunzo hayo ni kuhamasisha na kuchochea kasi ya ongezeko la wananchi wengi zaidi kutambua haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa kwa uratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mpaka sasa shirika hilo linaendelea kutoa mafunzo hayo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye majimbo ya Singida Mjini, Singida Vijijini, Singida Kaskazini, Singida Magharibi, Manyoni Mashariki, Iramba Mashariki na Magharibi.

“Tunapita kwenye mikusanyiko na kufanya mikutano na wananchi na kuwapatia elimu hii ya uraia, na  tunashukuru kila tunapopita mwamko ni mkubwa. Ujumbe wetu mkubwa kama shirika la WOWAP ni kuwasihi wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura wasipoteze fursa hiyo muhimu ifikapo Oktoba 28,” alisema Afisa Utawala wa Shirika hilo, Loveness John. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com