Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA TANO ZATEMBELEA MIRADI YA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO INAYOTEKELEZWA NA SHIRIKA LA ICS

 Kiongozi wa msafara wa Wizara tano, Sifuni Msangi, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akilipongeza shirika la ICS kwa nzuri ambayo wanaifanya ndani ya jamii katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia

Na Marco Maduhu - Shinyanga. 
Serikali kupitia Wizara tano, imetembelea miradi ambayo inatekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Investing in Children and Societies (ICS Africa) ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii, likiwemo tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Ziara hiyo imefanyika Jumatatu Oktoba 12,2020, kwa kutembelea miradi ya vikundi vya wasichana, wazazi, walimu, pamoja na kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), ambavyo vilipewa elimu ya malezi bora, pamoja na kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii. 

Wizara tano ambazo zimetembelea miradi hiyo ya Shirika la ICS, ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI. 

Akizungumza kiongozi wa msafara huo Sifuni Msangi, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema wametembelea miradi hiyo ili kujionea uhalisia wa kazi zinazofanywa na Shirika la ICS, katika kutekeleza mpango mkakati wa kitaifa wa Serikali wa kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA). 

Amesema amefurahishwa na Shirika hilo namna linavyofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kupambana kutokomeza matukio ya ukatili ndani ya jamii, ikiwamo kupigania ndoto za wanafunzi kwa kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni. 

"Shirika hili la ICS ni mfano bora sana wa kuigwa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kwa utendaji wake kazi, ambapo tumetembelea miradi yao na kuridhishwa na kazi zao ambazo wanazifanya ndani ya jamii ya kutokomeza matukio ya ukatili zikiwamo mimba na ndoa za utotoni," amesema Msangi. 

Mwenyekiti wa moja ya kikundi cha mabinti ambao wamepewa elimu ya ukatili kutoka kijiji cha Mwantini, Mary George, amelipongeza Shirika hilo kwa kuwapatia elimu ya kujitambua, pamoja na kuwajengea uwezo namna ya kufuga kuku na kujiwekea hisa, fedha ambazo zitawasaidia kutimiza mahitaji yao ya shule na kutojiingiza kwenye vishawishi. 

Naye mwenyekiti wa kikundi cha wazazi Eva Joseph, amesema Shirika hilo limekuwa msaada mkubwa sana kwao, ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ukatili ndani ya jamii. 

Mkurugenzi wa Shirika la ICS Kudely Sokoine, amesema wanatekeleza miradi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania (WFT), halmashauri ya Shinyanga na Ofisi ya mkuu wa Mkoa Shinyanga kwa kutoa elimu ya malezi bora na ukatili kwa wazazi, pamoja na wanafunzi kujitambua na kutoa taarifa dhidi ya matukio hayo. 

Amesema mbali na kutoka elimu hiyo ya ukatili, pia wamekuwa wakivijengea uwezo vikundi hivyo, namna ya kujikwamua kiuchumi kwa kufuga kuku, pamoja na kilimo, sanjari na kuzijengea uwezo asasi nyingine za kiraia zikiwamo na Kamati za MTAKUWWA. 

Pia amesema katika mpango kazi wao wa Shirika hilo kwa mwaka (2020-2021), wamejipanga kutoa elimu ya malezi bora na ukatili kwa wazazi 1,446 , walimu 160, pamoja na watoto 500,walio shuleni pamoja na nje ya shule, lengo likiwa ni kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Kiongozi wa msafara wa Wizara tano, Sifuni Msangi, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akilipongeza shirika la ICS kwa nzuri ambayo wanaifanya ndani ya jamii katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia

Mkurugenzi wa Shirika la ICS Kudely Sokoine, akisoma taarifa ya Shirika hilo juu ya miradi ambayo wanaitekeleza katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii. 
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Usule Geofrey Mateko, akitoa pongezi kwa Shirika la ICS namna lilivyowajengea uwezo na kufanikiwa kupungua kwa matukio ya ukatili shuleni hapo.
Mzazi Shija Ng'oma, akielezea namna elimu ya malezi bora ilivyosaidia kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii dhidi ya wanawake na watoto, likiwamo na suala la kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni.
Wageni kutoka Wizara Tano wakisikiliza mafanikio ambayo yametokea ndani ya jamii, mara baada kupewa elimu ya malezi bora na kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake Chimbuko la maendeleo kutoka Bukene,Eva Joseph, akielezea namna elimu ya kupinga matukio ya ukatili ilivyobadilisha maisha yao na kujawa na amani.
Wanakikundi cha wanawake Chimbuko la maendeleo kutoka Bukene, wakiwa kwenye kikao na wageni kutoka wizara tano.
Wageni kutoka Wizara tano wakikagua miradi ya ufugaji kuku kutoka katika kikundi cha Furaha cha wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari na msingi Mwantini, ambapo pia kinajiwekea hisa, kwa ajili ya kupata fedha za kununua mahitaji yao ya shule.
Baadhi ya kuku wanaofungwa na wanafunzi hao kati ya kuku 40.
Mratibu wa MTAKUWWA mkoani Shinyanga Tedson Ngwale, akizungumza na wanafunzi hao na kuwataka wajikite kwenye masomo yao ili watimize ndoto zao.
Wageni kutoka wizara Tano wakipiga picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari na msingi Mwantini mara baada ya kumaliza kukagua mradi wao wa ufugaji kuku.
Walimu wakiwa kwenye kikao na wageni kutoka Wizara tano.
Walimu wakipiga picha ya pamoja na wageni kutoka Wizara tano, mara baada ya kumaliza kikao.
Wageni kutoka Wizara Tano wakifurahi pamoja na wanakikundi cha wanawake na chimbuko la maendeleo kutoka Bukene.
Wageni kutoka Wizara tano, wakipiga picha ya pamoja na baadhi ya viongozi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga pamoja na Shirika la ICS.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com