Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM jimbo la Shinyanga Patrobas Katambi
Na Suzy Luhende, Shinyanga
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM jimbo la Shinyanga Patrobas Katambi, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili aweze kuwaletea maendeleo ikiwemo kujenga soko kuu la Kisasa katika manispaa ya Shinyanga.
Hayo ameyasema leo kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo katika eneo la soko kuu ambapo aliwaomba wananchi wawachague wagombea wa kutoka Chama Cha Mapinduzi ili waweze kuwaletea maendeleo.
"Mimi kazi yangu ni kusimamia maendeleo naombeni mnipe ridhaa muwape ridhaa madiwani wote wa jimbo hili, mmpe kura zote Magufuli ili tuweze kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hili ",amesema Katambi.
"Mimi kwa kweli napenda kusimamia haki ya wananchi na nitahakikishia nasimama imara, nitumeni muone jimbo letu litakavyobadilika .Nitahakikisha akina mama wanajikwamua kiuchumi kwa kupatiwa mikopo, vijana watajikwamua kiuchumi kwa kupatiwa mikopo, walemavu nao wana fungu lao lazima walipate ili na wao waweze kufanya biashara waweze kujikwamua kiuchumi", amesema Katambi.
Amewaomba wananchi wampe kura za kutosha awe Mbunge akieleza kuwa ana uwezo wa kupambana usiku na mchana ili kuliletea maendeleo jimbo la Shinyanga.
Kwa upande wake Mjumbe wa halmashauri kuu NEC Gasper Kileo ambaye pia ni kampeni meneja wa mgombea ubunge Patrobas Katabi amesema wananchi wasikubali kushawishika na kukipa kura chama cha upinzani kwa sababu hakitaleta maendeleo yoyote katika jimbo hilo.
"Nawaombeni sana wananchi wenzangu tusidanganyike tukakipa kura chama cha upinzani tukipe kura chama tawala kwa sababu ni chama cha wazalendo ni chama kinacholinda amani, tuchague madiwani Rais Magufuli na katambi ambaye ndiye simba dume la jimbo la Shinyanga"amesema Kileo.
"Tusikubali kuchagua chama cha upinzani , tukichagua upinzani tutarudi utumwani, si mnakumbuka babu zetu walitundikwa kwenye miti, wakati wa ukoloni, nchi yetu mpaka sasa inasimamiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi, CCM ina amani tusikubali tusije tukatendwa vibaya" aliongeza Kileo.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa amesema anawaomba wananchi wawapigie kura madiwani wote mbunge wa jimbo hilo na za Rais Pombe Magufuli kwa sababu chama hicho kimetekeleza maendeleo mbalimbali 2015, hivyo ndiyo maana kura zote za watanzania wote wa Shinyanga zinatakiwa kupigiwa CCM.
"Wapeni kura zote kwa kishindo diwani Gulam Hafeedh na mbunge wanu Patrobas Katambi na Rais Pombe Magufuli ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuijenga Shinyanga",amesema Mabala.
Social Plugin