Na Damian
Masyenene, Shinyanga
Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (CCM) amewashukuru wananchi wa mkoa wa Shinyanga kwa kumuamini na kumchagua kwa kura za kishindo dhidi ya wapinzani wake, ambapo amewaahidi kuwa hatokuwa mbunge dhaifu na endapo ataenda kinyume na matarajio ya wananchi basi wamuondoe.
Katambi
ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2020 mchana katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini wakati akiwashukuru wanachama, mashabiki,
wakereketwa na wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kwa kura nyingi jana wakati
wa zoezi la upigaji kura.
Katambi
alitangazwa mshindi wa ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kwa kupata kura 31,831
dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Salome Makamba wa Chadema aliyeambulia kura
16,608.
Akizungumza na maelfu ya Wana CCM na wananchi waliojitokeza katika mkutano wake huo wa kutoa shukrani kwa wapiga kura, Katambi ameeleza kuwa sasa analo deni kubwa mbele ya wananchi waliomuamini na kwamba atakwenda kuchapa kazi usiku na mchana.
“Tumefanya
uchaguzi wa kihistoria na Shinyanga mmeonyesha mfano, siwezi kutumia nafasi
mliyonipa kwa kusaka umaarufu binafsi na mali….ambao hawajanipigia kura
wamenipa nafasi ya kuwadhihirishia kwamba mimi ni bora na wakati ujao
wataniunga mkono.
“Naomba
Mungu anisaidie nikawe kiongozi wa mfano nisije nikawadhalilisha wana
Shinyanga, lazima tuelewane mapema atakayetafuna fedha za miradi nitakula nae
sahani moja….na nawaomba nikizingua msisite nipigeni chini wekeni mtu mwingine
wananchi wanataka maendeleo, na ikitokea diwani hafuati sheria na taratibu za
chama na akatumia cheo kwa maslahi binafsi tutampiga chini, lazima tubadilike
tulete maendeleo na tuchape kazi,” amesema.
Katika hatua
nyingine, Katambi amesema yote yaliyotokea wakati wa kusaka kura yamekwisha na
kuwaomba wanasiasa wenzake kuyasahau, ambapo amewasamehe wote waliomtukana na
kumdhalilisha, hivyo hivyo akawaomba na wao wamsamehe pale alipowakosea.
“Yeyote
aliyenikosea na kunidhalilisha nimemsamehe bure na wote niliowakosea na
kuwakera basi wanisamehe pia….pia nawaomba wananchi mtukosoe na kutushauri kwa
nia njema ya kujenga, msije mkanisifu tu kunivimbisha kichwa,” ameeleza.
"Nawashukuru sana kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, nawapongeza sana kwa sababu hamkuchagua Mbunge Boya 'dhaifu'. Hakika tukishirikiana pamoja tutaibadilisha Shinyanga. Ushirikiano wenu ndiyo nguzo muhimu ya kufikia maendeleo tunayotaka",ameongeza Katambi.
Katambi pia
aliongozana na washindi wa nafasi za udiwani katika kata 17 za jimbo hilo,
wakiwemo Gulam Hafeez Mkadam wa Kata ya Mjini, Mariam Nyangaka wa Kitangiri,
Ruben Masanja wa Lubaga na madiwani wapya ambao wamezikomboa kata zilizokuwa
upinzani akiwemo Zamda Shaban wa kata ya Ndala pamoja na Victor Mkwizu
(Ngokolo), ambao wamewashukuru wananchi kwa kuwaamini, huku wakiahidi
kuwatumikia wananchi na kuibadilisha Shinyanga.
Kwa Upande
wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC), Gaspar Kileo maarufu GAKI ambaye alikuwa Meneja
Kampeni wa Katambi amewashukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kukiamini Cha Cha
Mapinduzi (CCM) kwa kukipa madiwani wote wa kata 17 na Mbunge na kwamba kazi
yake ameimaliza kwa mafanikio, sasa anakiachia chama kuhakikisha wateule hao
wanatekeleza ilani ya chama hicho kwa vitendo kama walivyoahidi.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akizungumza na maelfu ya wananchi wa Shinyanga kwa njia ya Simu kupitia simu ya Meneja Kampeni Gaspar Kileo amewashukuru wananchi kwa kuendelea kuiamiani CCM na kuchagua wagombea wote.
"Shinyanga Mjini mmetia fora, asanteni sana kwa kuchagua Madiwani wote wa CCM, Mbunge wa CCM na hatuna wasiwasi kuhusu Mgombea Urais Dk. John Pombe Magufuli najua naye mmempa kura za kutosha",amesema Mlowa.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Social Plugin