Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Hamis Kulemba
Na Sitta Tumma, Simiyu
Idara ya Afya mkoani Simiyu, imeziagiza halmashauri za mkoa huo, kuunda vikosi maalumu vya kutoa elimu kwa jamii, namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, ikiwamo ujengaji wa vyoo.
Ripoti ya kitaalamu katika mambo ya afya inasema, hadi sasa asilimia 98 ya kaya mkoani hapa zina vyoo, kati ya hizo, asilimia 60 ni vyoo bora.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Hamis Kulemba, katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi, amesema jamii ya pembezoni lazima ifikiwe na elimu hiyo.
Amesema elimu inayotakiwa kumfikia mwananchi ni kutokujisaidia ovyo vichakani, kutunza vyanzo vya maji, kujenga choo na kukitumia, kunawa mikono, kuchemsha maji ya kunywa nakadhalika.
"Hadi sasa Mkoa wetu wa Simiyu una ziro ripoti ya magonjwa ya mlipuko. Ndiyo.
"Lakini hatuwezi kubweteta. Lazima timu za kupambana na magonjwa yakiwamo ya mlipuko zitilie mkazo mambo haya," Dk. Kulemba amesema.
Kulingana na mtaalamu huyo wa masuala ya afya, jamii ijenge mazoea ya kunawa mikono mara kwa mara.
Uchunguzi unasema, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi na sabuni, kunaondoa asilimia 75 ya uwezekano wa raia kupata magonjwa ya mlipuko.
"Tumejidhatiti. Magonjwa ya mlipuko ikiwamo kuhara damu, kuharisha na kipindupindu tunapambana nayo kuyadhibiti.
"Katika ugonjwa wa uti wa mgongo unaoambukizwa kwa njia ya hewa, tuhamasisha watu kujenga nyumba zenye madirisha yanayopitisha hewa vizuri," amekaririwa Dk. Kulemba.
Helen Maduhu, Mboje John, Saguda Ndulu na Ester Sitta, wakazi wa Bariadi, Simiyu, wameshauri elimu hiyo ya kujikinga na magonjwa itolewe hadi shuleni.
"Haya magonjwa yanaua," ametahadharisha Edina Edward, mkazi wa Somanda, Bariadi.
Social Plugin