MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amewaomba kura maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala ambao wamefika katika mkutano wake wa kampeni huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mambo muhimu yanayohusu Taifa la Tanzania.
Ametumia nafasi hiyo kufafanua hatua kwa hatua nchi yetu ilikotoka,iliko na inakokwenda ambapo amewataka Watanzania kushikamana na kuwa wamoja kwani hivi sasa nchi iko kwenye vita ya kiuchumi na kuna mataifa makubwa yanachukia wananapoona maendeleo makubwa yanayofanyika hivi sasa chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi hao wa Wilaya ya Ilala ambao wanawakilisha majimbo ya Ukonga, Segerea na Ilala katika mkutano huo wa kampeni za kuomba ridhaa ya miaka mitano mingine, Dk.Magufuli amewaambia wananchi hao Dar es Salaam anaifahamu vizuri na ameishi katika Jiji hilo kwa zaidi ya miaka 30 tangu akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu ,baadae Serikalini akiwa Waziri na sasa akiwa Rais.
"Ndugu zangu nimeishi Dar es Salaam miaka mingi sana, miaka yangu ya uwaziri ni 20 yote nimeishi hapa, maisha yangu ya kusoma wakati nikiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikuwa hapa, miaka yangu karibu mitano ya Urais kabla ya kuhamia Dodoma nimekuwa hapa.
"Ninachotaka kuwaambia Dar es Salaam ninajua vizuri, ahadi ambazo nilikuwa nazitoa nilikuwa nafahamu , nataka kuibadilisha na hayo ndio yalikuwa malengo yangu.Baada ya uchaguzi mwaka 2015 mlichagua CCM na maeneo mengine mkachanganya, mlipochanganya, mkawa mmenipa break ya kufanya kazi, ni kama vile mmenichagua mimi nenda halafu mmenifunga miguu. Nafahamu mlivyokuwa mnahangaika katika mambo.mbalimbali,"amesema Dk.Magufuli.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake mambo yamebadilika, maendeleo yamepatikana kwani wamejenga daraja la Kinyerezi, wamejenga barabara za lami na kuboresha huduma za kijamii kama afya,elimu na umeme.
Hata hivyo amesema kutokana na kuchanganya na wabunge na madiwani kutoka vyama vya upinzani, kuna maendeleo.ambayo yamechelewa kupatikana akitolea mfano ujenzi wa stendi ya Mbezi Luisi iliyochukua miaka kadhaa kupata mkandarasi , hivyo ilibidi niingilie kati.
"Wana Segerea ,Ilala na Ukonga mmejifunza, kufanya kaso ni kosa ili kufanya kosa ni kosa zaidi.Katika kipindi cha miaka mitano ijayo naomba mnichague mimi kwa nafasi ya Urais , madiwani na wabunge wawe wa CCM halafu tukikwama mje mniulize.
"Maendeleo hayana Chama na ndio maana katika mkutano huu wa kampeni watu wa vyama vyote wapo hapa.Kila kabila wako hapa, unaweza kuiona Tanzania, ndio maana naomba tujenge umoja wetu.Taifa letu wengi wanalionea gere na nitawaambia kwanini wanaona gere
"Mwaka 1885 mataifa ya Afrika yaligawiwa kwa Wazungu, yaligawanya kwa vipande, Tanzania tulitawaliwa na Wajerumani na baadae Waingereza, kwa miaka mingi tukawa vibarua, Tanzania ilikuwa kama sehemu ya kuzalisha malighafi na kisha kupelekwa Ulaya.Ukishapeleka malighafi maana yake umepeleka ajira kwao.
"Ilipofika mwaka 1961 baada ya Mwalimu Nyerere kushika madaraka alikuwa na kazi ya kulijenga Taifa kuwa moja, nchini kwetu tuna makabila 121 lakini tuliunganishwa na Mwalimu, alilijenga taifa la Tanzania na katika kulijenga akaungana na Zanzibar na ndio Tanzania ikaundwa.
"Kila Mtanzani atambue wako katika taifa huru, na kuwa huru ni jambo moja na kuwa huru kiuchumi ni jambo jingine, tuliingia vita vya Uganda kati ya mwaka 1978 na mwaka 1799, wakati huo hata ukikamawata na sports man unaambiwa mlanguzi, akaja mzee ruksa, baada akaja mzee mkapa akaendelea kujenga nchi, ndio aliyesababisha tusamehewe madeni, mimi nilikuwa Waziri wake wa ujenzi kwa miaka 10, nafahamu jinsi ambavyo barabara zilikuwa hazijengwi. maneo mengi hayakuwa na barabara za lami,amesema Dk.Magufuli.
Amefafanua baada ya Mzee Mkapa muda wake kwisha, aliingia Mzee Kikwete, anafahamu changamoto ambazo Kikwete amekumbana nazo kwani yeye alikuwa waziri wake na hakuwa akitegemea kuna siku atakuwa rais, lakini sasa amekuja yeye."Nilipata urais bila kuhonga wala kutumwa na mtu, naamini nimepata nafasi hii kutoka kwa Mungu na ndio maana kauli mbiu yangu ikawa Hapa kazi tu.
"Wakati tunaingia madarakani hakukua na amani, Kibiti walikufa watu wakiwemo askari polisi 17 waliuawa, kule Kigoma nako hakukua salama, watu walikuwa wanaiba mchana.Pale Ubongo saa sita mchana mtu aliingia kuiba, lakini katika utawala wangu nimekomesha. wakati naingia madarakani watu walikuwa wanakuja dukani na kukwambia tunakuja kuchukua fedha zetu, na kweli wanachukua.
"Hivyo nilihakikisha tunajenga amani ya Watanzania, nafikiri hili tumelifanya vizuri, najua bado kuna changamoto lakini ndio maana tunaomba tena kura ili tukashughulikie.Ndugu zangu mnafahamu hali ya mazingira, barabara zilikuwa ni shida, pamoja na kukwamisha na wale waliokuwa wameshika Jiji lakini tulifanya baadhi ya maendeleo,"amesema.
Amewakumbusha wananchi hao mkataba wa ujenzi wa barabara ya juu Tazara aliusaini akiwa katika kampeni za mwaka 2015, watu walikuwa wanakaa muda mrefu na wengine kutumia nafasi hiyo kuongopa kwa familia.
"Katika utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia Sh.bilioni nne zilikuwa zinapotea kila siku kwasababu ya foleni, nikasema hili haiwezekani lazima tumalize tatizo.Tulianzisha treni ya Mwakyembe kwa mwaka inabeba watu milioni sita. Mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam ambao unajulikana kama DMDP zimetengwa Sh.bilionii 660 na bado unaendelea.
"Na ndio maana ndugu zangu wana Segerea, Ukonga na Ilala tunakuja kuomba kura ili katika miaka mitano ijayo tufanye maajabu.Ninafahamu kuna mambo mengi yamefanyika katika majimbo haya. hata suala la suala la wajasirimali limeelezwa, sio siri wajasiriamali walikuwa wananyanyasika, kila mahali wanafukuzwa, ilikuwa bora ukutane na Simba kuliko mgambo, ukiwa na viazi wanamwaga, ukiwa na uji wana kunywa, na wakati mwingine wanabeba wanapeleka nyumbani.
"Hata kwa Mkurugunzi naye ni hivyo hivyo, hadi wajasiriamali wakawa wanajiuliza hivi nao ni wa Dar es Salaam, nikasema dawa yake ni ndogo nikaamua kutengeneza vitambulisho vya Rais na nilisema vitambulisho vya rais ili watu wasinyanyasike. Watu walikuwa wanalipa 1000 kwa siku na kwa mwezi 30, 000.
"Hivyo kwa mwaka gharama ni kubwa, lakini kwa kuwa wanachi hawa wanyonge walinichagua nakasema kitambulisho kitakuwa 20,000, kitambulisho ambacho unafanya biashara mahali kokote, hivi ndugu zangu nilifanya vibaya kuwapa vitambulisho.Kitambulisho kinamfanya mjasiriamali kuwa huru na nchi yake,"amesema.
Ameongeza kuwa mkakati uliopo wanataka watu wawe wanapata mikopo kwa kutumia kitambulisho hocho kwani halmashauri zinatoa mikopo kwa vijana,walemavu na wanawake, hivyo ukienda na kitambulisho hicho kwenda kukopa,unakopeshwa.
"Nimewapa wafanyabiashara wadogo jeuri ya kuishi bila kubudhiwa, sasa kwasababu ya kisiasa watu ambao walizunguka na kulitukana hili taifa leo wanakuja wanasema vitambulisho havisaidii, wakashindwa wakalege.Hawalijui hili taifa, taifa hili limesimama kutokana na misingi mizuri iliyoachwa na waasisi wetu, nchi hii ni matajiri, tulikuwa tunaambiwa nchi hii masikini huku wanasomba dhahabu,
"Nilipoingia madarakani nikawaambia Tanzania ni tajiri kuliko hata kwa Wazungu, nilipoingia tukaanza kubana mianya ya fedha tukanunua ndege 11, tumejenga jengo la abiria uwanja wa ndege wa kimataifa Dar es Salaam, tumejenga barabara, tukaanza kutoa elimu kwa watoto wetu kuanzia la kwanza hadi sekondari bure, hata Ulaya hawafanyi hivyo, wanalipa hela, hivyo tunapofanya hivi wanuna, wanaona gere, hata bajeti ya fedha kwa ajili ya chuo kikuu imeongezeka.
"Tuliamua kuanza kujenga vituo vya afya na zahanati, tumejenga hospitali za rufaa, tumejenga hospitali za mikoa,tumejenga hospitali za Wilaya. Wanaona gere, wanaona viwu, wanaona uchungu, walikuwa wanatuuzia umeme, ukienda Kariakoo majenereta yalikuwa mengi yanashindana kulia kama Bongo Fleva, tukasema hapana , nchi hii ina vyanzo vingi vya umeme.
"Tukaamua kuanza na bwawa Julius Nyerere na tulipoanza kuzungumza wakasema tunaharibu mazingira, tulipoenda kuchunguza tukakuta kule wamejenga hoteli, wamejenga viwanja vya ndege, wanachukua meno ya tembo.Tukasema tunajenga bwawa, tulipoomba fedha wakakataa, sasa tunajenga kwa fedha zetu, tunataka umeme ukasambae kila mahali, palipo na shida ya umeme ukaingie, na tunataka bei ya umeme ishuke chini, kama wanavyouziana wao, wakiona haya yote hawawezi kufurahi,"amesema Dk.Magufuli.
Amesisitiza anaeleza ukweli na hiyo ndio sadaka yake kwa Wana Dar es Salaam, kwa hiyo Watanzania walishikwa kiuchumi,hivyo kiuchumi walikuwa bado hawajajikomboa."Tanzanite walikuwa wanasomba usiku na mchana, tulikuwa kwa mwaka tunapata asilimia nne tu, nchi iliyokuwa inaongoza kwa kuuza Tanzanite haikuwa Tanzania.
"Tukaamua kujenga ukuta, niliposema najenga ukuta waliniona kama kichaa, Tanzanite yote iko ndani na tumefunga kamera, ndio maana mnaona akina Laiza wanakuwa mabilionea.Tukaja kwenye dhahabu, wameiba makontena na makontena wanapeleka Ulaya, walikuwa wanasomba na mchanga wote.
"Kama mchanga tu kwanini usitumike kujenga daraja la Kiinyerezi, wameiba sana, mikataba inasainiwa Ulaya bila Watanzania kujua. nimekuwa serikali najua , niliamua kubadilisha, walikuja wakasema serikali itafungwa, hatuwezi kushindana na Wazungu. hao Wazungu wameshaachia gawio la Sh.bilioni 100 na kesho wanaleta tena Sh.bilioni 100 nyingine na fedha hizo ndio hizo tunazitumia kujenga barabara, kulipa ada na kufanya maendeleo mengine nchini kwetu,"amesema.
Ameongeza kuwa wanapotoa fedha hizo sio kama wanapenda , wanazitoa kwa shida na adui yao namba moja ni yeye( Rais Magufuli)ambaye anakwamisha, hawawezi kumfurahia."Tukaja kwenye Corona , wakataka watu wote tufungiwe ndani, tukaambiwa tuwe tunavaa barakoa,ukiwa na bodaboda ukae ndani, dukani usiende, shambani usiende
"Katika kipindi ambacho nilipata ugumu ni hapo, nikasema ngoja nimuombe Mungu wangu anipe majibu, nikasema ngoja nitumie hii elimu ambayo walinipa wao, nikapima papai lina Corona, nikapima Kware wana Corona nikajua huu ni mchezo wa kuliangamiza taifa.Tukafunga kwa siku tatu na kumshukuru kwa siku tatu, Mungu ameondoa Corona, msifikiri wanafurahi, walitaka kuuza madawa yao, walitaka kutuuzia mavifaa yao, walitaka tutumike kama wanyama kupima madawa yao, nimewakwamisha, Watanzania wamewakwamisha.
"Wakaja na kutaka kutupa na mkopo wakati huo wa Corona nikawaambia waondoke na mikopo yao kwani sisi tunafanya kazi, wengine wameanza kuiga kwa kumuomba Mungu, na kwa Mungu hakuna kinashindikana. Wakati huo wa Corona uchumi wetu ukawa unapanda na wao wenyewe wakatutangaza nchi yetu sio masikini tena,"amesema Dk.Magufuli.
Amewaambia wananchi kwamba sasa mambo mazuri yanakuja, hivyo maadui watatumia mbinu za kila aina , watatuma wasasiliti, watatuma watu wa kututakana lakini anaamini watanzania wataendelea kuwa wamoja na anawaomba wasimame imara kama Taifa.
"Sisi wote ni watanzania, tuko kwenye vita ya uchumi wa kulijenga taifa , hivi ukiwa na kocha mzuri na umepandisha timu kutoka daraja la pili hadi la kwanza huyo kocha mnambadilisha au unamuacha.Wilaya ya Ilala iko kati kati ya Jiji, ina watu wengi, ina changamoto nyingi, hivyo niko mbele yenu kuwaomba mniletee hawa wabunge, ili nibaki na deni kwenu, kwamba mniulize tulikupa madiwani na wabunge mbona hiki hakijafanyika.
"Nileteeni ndugu zangu wabunge na madiwani mimi nawajua hawa, wamepitishwa vizuri wamechujwa, wamechujwa kamati kuu, wamechuhwa halmashauri kuu, wamechujwa kwenye mikoa yao na wilaya.Nipenii hawa ili nitimize dhamira yangu bila vikwazo.Katika miaka mitano inayokuwa tutaboresha zaidi, katika miaka mitano inayokuja fly over 11 zitajengwa, Dar itakuwa kama Ulaya na tutawazidi kwani tunakila kitu, tuna bandari tatu Tanga, Dar na Mtwara.
"Tunajenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi nchini Uganda kuja Tanga lenye urefu wa kilometa 1445. Bomba linakopita kote ni pesa, ule mradi ungeenda mahali kwingie lakini tumesimama imara.Katika miaka mitano tumejenga viwanda 8447 na jirani zenu Pwani ndio wanaongoza kwa viwanda vingi.Hiyo ndio Tanzania mpya ambayo tunataka kuijenga,"amesema.
Amefafanua mwaka huu wameapanga kufufua miradi mingi zaidi,hivyo amewaomba wananchi kuwachagua wagombea wa CCM ili akafanye nao kazo na sio kumpelekea wabunge asiowajua." Ninafahamu kuna maneo yenye mafuriko katika Wilaya hii ya Ilala lakini tayari Sh. bilioni 32 zimepanwa kwa ajili ya mradi huu,"amesema Dk.Magufuli huku akifafanua jinsi mabilioni ya fedha yalivyotumika katika miradi mbalimbali ya kijamii.
CHANZO - MICHUZI BLOG