Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTOTO AUNGUZWA MIKONO BAADA YA KUIBA SH. 400 YA SADAKA YA MAMA YAKE!

 JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa linamshikilia mkazi wa eneo la Kaloleni lililopo Manispaa ya Sumbawanga, Stella Kangoza (29) kwa kuichoma moto mikono ya binti yake mwenye umri wa miaka tisa akimtuhumu kumuibia Sh 400 aliyopanga kutoa sadaka katika ibada ya Misa Takatifu Jumapili iliyopita.


Msichana huyo anasoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Chemchem iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa Jumapili iliyopita Stella alipokuwa akijiandaa kwenda kusali alipekua alipoweka fedha Sh 400 za sadaka na hakuziona hivyo hakutoa sadaka kanisani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo alithibitisha kutokea kwa mkasa huo na kwamba ni kitendo cha ukatili na kwamba mama huyo amemsababishia binti yake ulemavu.

Akifafanua zaidi Kamanda Masejo alisema kuwa mama huyo alitenda ukatili kwa binti yake saa mbili usiku wa Jumapili iliyopita nyumbani kwake katika eneo la Kaloleni lililopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Alieleza kuwa binti huyo amelazwa hospitalini kwa matibabu na kuwa hali yake imeanza kuimarika na kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali wa shauri lake kukamilika.

“Taarifa kutoka kwa raia wema zilifanikisha kutiwa nguvuni kwa mtuhumiwa huyo,” alisema Kamanda Masejo.

Kamanda Masejo aliwaonya vikali wananchi hasa wazazi wachache wanaotumia nguvu kutoa adhabu kwa watoto wao na kuwataka washirikiane na Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto ili kuhakikisha jamii inakuwa na kizazi salama kisicho na uhalifu.

Aliitaka jamii iendelee na moyo huo huo wa kutoa taarifa au viashiria vya uhalifu na kuwaripoti wote wanajihusisha na vitendo vya kihalifu ili hatua dhidi yao zichukuliwe na kuwa fundisho kwa wengine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com