Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Mariam Julius (26) mkazi wa Kitongoji cha Danduhu A kijiji cha Didia kata ya Didia wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na mmewe aitwaye Eliya Paul Shija (30) ambaye naye amejijeruhi kwa kujichoma kisu tumboni akitumhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine 'kuchepuka nje ya ndoa'.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema tukio hilo limetokea saa saba usiku wa kuamkia leo Jumapili Oktoba 11,2020 nyumbani kwa wanandoa hao katika Kitongoji cha Danduhu,kijiji cha Didia wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Mwenyekiti wa Kijiji cha Didia, Mrisho Hamad amesema mwanaume huyo baada ya kumuua mke wake ndani ya nyumba waliyokuwa wanaishi naye alijichoma kisu tumboni na kuacha ujumbe wa maandishi ambao umechukuliwa na Askari polisi waliofika eneo la tukio.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari Jeshi la polisi linamshilikilia mtuhumiwa Eliya Paulo Shija (30) baada ya kumuua mkewe aitwaye Mariam Julius (26),wote wakazi wa Didia na kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi.
“Mnamo Oktoba 11,2020 majira saa saba kamili usiku katika kijiji cha Didia, kata ya Didia, tarafa ya Itwangi, wilaya ya Shinyanga vijijini na mkoa wa Shinyanga, Mariam Julius akiwa chumbani amelala aliuawa kwa kuchomwa kisu sehemu za shingoni na mtuhumiwa mume Eliya Paulo Shija, ambaye naye kwa sasa ni majeruhi ambapo baada ya kumchoma kwa kisu mkewe naye alijichoma kisu sehemu za tumboni na kusababisha utumbo wake kutoka nje”,anaeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema Chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu mkewe kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine ambaye hamjui kwa jina wala kwa sura akidai kuwa watu ambao huwa wanashirikiana kumtafutia wanaume (MAJINA TUNAYAHIFADHI),wakazi wa kijiji cha Didia.
Kamanda Magiligimba amebainisha kuwa taarifa hizo amezitoa mtuhumiwa kwenye ujumbe wa maandishi uliokutwa kwenye daftari chumbani mwao na majeruhi ambaye ni mtuhumiwa inasadikika alijichoma kisu tumboni kwa lengo la kujiua na hali yake ni mbaya sana na amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa matibabu zaidi.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga ukisubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Kamanda huyo wa polisi ametoa wito kwa kuendelea kusisitiza kuwa wenzi/wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wapeleke matatizo/migogoro yao ya ndoa kwenye ofisi za dawati la jinsia na watoto, viongozi wa dini, ofisi za ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao.