Mgombea Udiwani kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu
Na Suzy Luhende - Shinyanga
Mgombea udiwani kata ya Ngokolo mjini Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Victor Mkwizu amesema akichaguliwa, kuwa diwani kipaumbele chake ni kujenga kituo cha afya katika kata hiyo.
Akizungumza jana wakati akinadi sera zake katika mtaa wa Majengo Mapya eneo la Sokoni Mkwizu amesema kata ya Ngokolo haina kituo cha afya, hivyo anawaomba wananchi wote wampe kura ili aweze kusimamia kituo cha afya kijengwe kwa kuwa wananchi wanapata shida wanapougua wanaenda kutibiwa kwenye kata zingine.
Pia amesema akichaguliwa atahakikisha wazee wa kata hiyo wanapata huduma za afya bure ambapo wataorodheshwa katika mitaa yote ili waweze kuhudumiwa bure bila malipo yoyote.
Aidha amesema kilichomsukuma kugombea udiwani ni barabara kuwa mbovu hazipitiki wakati wa mvua hivyo atahakikisha anaondoa kero ya barabara ataweka sehemu ya vivuko pale panapohitajika, ataweka madaraja pale panapohitajika, pia atajenga kituo cha polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama katika kata hiyo.
"Naombeni mnichague mimi Victor Mkwizu kutoka CCM ili niweze kuwatumikia, nitumeni wazazi wangu nitumeni ndugu zangu naamini sitawaangusha, nitakuwa nanyi mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maendeleo yetu ya kata ili kujua kuna tatizo wapi kuna kero wapi naombeni ridhaa yenu,"amesema Mkwizu.
Katika sekta ya michezo amesema ataanzisha mashindano ya mbio za baiskeli, filamu, muziki, uchoraji ambapo ataandaa mashindano ili vijana wa kata hiyo waweze kuinua kipato chao.
"Nitakaa na maafisa mipango Miji ili tuweze kupitia na kufanya miundombinu ya soko na kuhakikisha inakuwa rafiki na ya kuvutia, kwani kuna wadau mbalimbali tutazungumza nao ili kuhakikisha tunafanikisha,"amesema Mkwizu.
Kwa upande wake,Kada wa CCM Jackline Isaro amewaomba wananchi wa kata ya Ngokolo wamchague Victor Mkwizu ili aweze kuwaletea maendeleo kwani ni kijana ambaye anajituma ni mpenda maendeleo.
Naye Mdau wa Maendeleo Godfley Mallya amesema Victor ni mpenda maendeleo na ni mkazi wa kata ya Ngokolo katika mtaa wa Majengo hivyo anazijua kero zote za kata, kwa sababu na yeye zimekuwa zikimkera hivyo amewaomba wananchi wamchague ili aweze kuondoa kero hizo.
"Ndugu zangu tusijidanganye tukachagua vyama vingine ambavyo mpaka sasa vilikuwa madarakani katika kata yetu lakini havijafanya maendeleo yoyote tunaona barabara ni mbovu, kituo cha afya hatuna, kituo cha polisi hatuna, wazee wetu wakifika hospitali wanapata shida hivyo tuchague diwani wa kuweza kuondoa kero zote hizi ndugu zanguni"amesema Godfrey Mallya.
Mgombea Udiwani kata ya Ngokolo kupitia CCM, Victor Mkwizu akiomba kura kwa wananchi.
Victor Mkwizu akiwa nyumbani kwake mtaa wa Majengo kata ya Ngokolo akiwa na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi ambapo aliongozana nao baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara ili kufuta kauli ya baadhi ya watu wakiwemo wagombea wa vyama vya upinzani wanaodai kuwa siyo mkazi wa Ngokolo, kushoto anayezungumza ni Godfrey Mallya ambaye ndiye anashuhudia kwamba Victor ni mkazi wa Majengo na ni jirani yake wa karibu anamjua vizuri.
Victor Mkwizu akiwa nyumbani kwake mtaa wa Majengo kata ya Ngokolo akiwa na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi ambapo aliongozana nao baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara ili kufuta ule usemi wanaodai si mkazi wa Ngokolo, kushoto anayezungumza ni Godfrey Mallya ambaye ndiye anashuhudia kwamba Victor ni mkazi wa Majengo na ni jirani yake wa karibu anamjua vizuri.
Social Plugin