Wananchi wakiwa katika mnada wa Tinde wilayani Shinyanga kwa ajili ya kuuza na kununua bidhaa mbalimbali
Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ameufunga mnada wa Tinde ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kuuhamishia katika eneo lingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 30, lengo likiwa ni kutatua changamoto ufinyu wa eneo na mrundikano wa watu unaoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, huku eneo likiloachwa wazi likitarajiwa kutumika kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na stendi ya mabasi.
Akizungumza katika mnada huo Jumanne Oktoba 27,2020 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amepiga marufuku wafanyabiashara kupanga bidhaa zao na kufanya biashara pembezoni mwa barabara kuu na kuwaagiza viongozi wa mnada kushirikiana na polisi kusimamia kikamilifu hali hiyo isijirudie tena.
Mboneko pia amepiga marufuku magari ya abiria kushusha na kupakia pembezoni mwa barabara kuu na kuwataka madereva kuingia ndani katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kupakia abiria na mizigo ili kuondoa hatari inayoweza kujitokeza barabarani.
Amesema Serikali ina nia njema kwa wananchi na kudai kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha yenye tija huku akiwataka wajasiriamali wote wa mnada huo kuwa na viongozi katika kila kundi kulingana na biashara zao akitaja baadhi ya makundi kuwa ni wafanya biashara wa nguo za mtumba, viatu vya mtumba na spesho, mama lishe, wauza ng'ombe,mbuzi, wauza dawa za asili, mboga mboga, nafaka na kadhalika.
Mwandishi wa habari hizi amefika katika eneo hilo jipya la mnada na kukuta wananchi wakiendelea na shughuli za kibiashara kama kawaida baadhi wakiwa wameridhika, lakini wengine wakilalamikia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara kuvuruga utaratibu waliowekewa na kupanga bidhaa pembezoni mwa barabara kuu ya kuelekea Kahama hali ambayo imeonekana kuwanyima riziki walioko ndani ya mnada.
Mmoja wa wafanyabiashara wa nguo katika mnada huo, Gelard Mchau amesema kuhamishiwa mnada katika eneo hilo imewasaidia kupunguza mbanano uliokuwepo katika mnada wa awali lakini hofu yake ni wakati wa mvua kwa kuwa eneo hilo lilikuwa na majaruba ya mpunga.
Aidha wafanyabiashara wengine wameishukuru Serikali ya Wilaya ya Shinyanga pamoja na halmashauri kutoa eneo hilo bure hali ambayo imetoa nafasi pana kwa baadhi ya wajasiriamali kujiendeleza kiuchumi.
Nao baadhi ya viongozi na wasimamizi wa mnada huo akiwemo Christopher Malengo ambaye ni msimamizi wa minada kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamesema mnada huo kwa sasa utaingiza mapato makubwa kwa sababu umewekwa katika eneo zuri ambalo linamvutia kila anayepita katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza baada ya kuuzindua mnada wa Tinde katika eneo jipya
DC Mboneko akitazama bidhaa mbalimbali katika mnada huo
DC Mboneko akisisitiza jambo ambapo amepiga marufuku magari ya abiria kupakia pembezoni mwa barabara na wafanyabiashara katika mnada huo kujiepusha kupanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara kwani ni hatari endapo ajali itatokea.
DC Mboneko akiendelea na ukaguzi katika mnada huo
Mfanyabiashara akiuza mbuzi kwenye mnada wa Tinde
Akina mama wakiuza vyombo vya ndani katika mnada huo
Shughuli zikiendelea katika mnada wa Tinde
Biashara ya nyama choma ikiendelea
Mmoja wa wafanyabiashara akina mama katika mnada huo akiwauzia samaki wateja waliofika mnadani hapo
Mmoja wa wakazi wa Tinde akinunua nyanya katika mnada huo
Mfanyabiashara akisubiria wateja kununua bidhaa
Biashara ya ng'ombe mnadani hapo ikiendelea
Msimamizi wa minada kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Christopher Malengo akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali
Baadhi ya wafanyabiashara katika mnada huo wakizungumzia hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Shinyanga kuufunga mnada wa zamani na kuuhamishia eneo jipya lenye ukubwa wa kutosha, ambao wamepongeza hatua hiyo.
Kiongozi wa wafanyabiashara wa vyombo vya ndani mnadani hapo akielezea mambo mbalimbali
Social Plugin