Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : MAFUNZO KWA WASAIDIZI WA KISHERIA KUPIGA VITA UKATILI WA KIJINSIA SHINYANGA YAFUNGWA.... TAHADHARI YATOLEWA "VISHOKA WA SHERIA"

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
***
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo amewataka Wasaidizi wa Kisheria ‘Paralegals’ mkoa wa Shinyanga kuepuka kuwa ‘Vishoka wa Sheria’ kwa kujiepusha kufanya majukumu ya Wanasheria badala yake wajikite katika kushauri wananchi kufanya nini ili kupata haki zao zikiwemo za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Tarimo ametoa agizo hilo leo Jumanne Oktoba 6,2020 wakati akifunga mafunzo kwa wasaidizi wa Kisheria 60 mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),UNFPA na KOICA na kuratibiwa na PACESHI kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia. 

Mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku 6 yaligawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza la Wasaidizi wa kisheria kutoka Halmashauri ya wilaya ya Msalala na Kahama Mji yalifanyika kuanzia Oktoba 1,2020 hadi Oktoba 3,2020 na kundi la pili la Wasaidizi wa kisheria kutoka Halmashauri ya Ushetu na Kishapu lilipata mafunzo kuanzia Oktoba 4,2020 hadi leo Oktoba 6,2020 yalipofungwa rasmi na Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo 

Mwanasheria huyo alisema bado mkoa wa Shinyanga unakabiliwa na changamoto kubwa ya matukio ya ukatili wa kijinsia akibainisha kuwa Wasadizi wa kisheria wana nafasi kubwa ya kushiriki katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika jamii kwa kujiepusha kufanya kazi za wanasheria.

“Elimu ya ukatili wa kijinsia na elimu katika sheria yetu ya msaada wa kisheria mkaiishi na kuitumia. Nawaasa na kuwasihi msiwe vishoka, msiende ku - perform ‘kufanya’ kazi za wanasheria kwa sababu nyinyi mnatakiwa mtoe ushauri badala ya practice ‘kufanya’ mfano kutoa talaka,kuamua mgogoro wa ndoa hilo siyo jukumu la wasaidizi wa kisheria”,alieleza Tarimo. 

“Vishoka hatuwataki na pia naomba tumsaidie mtu katika moyo wa kweli maana yake wengi wanaotufikia hata uwezo hawana, naomba usimwambie akupe hata shilingi 5 au elfu 10,yeye mwenyewe hana, amekuja ni mjane,mwelekeze anatakiwa kufanya nini na msaada wake aupate wapi”,aliongeza Tarimo.

Mwanasheria huyo ambaye pia ni Afisa Malalamiko mkoa wa Shinyanga alitumia fursa kutahadharisha kuhusu kuibuka kwa wimbi la baadhi ya watu katika jamii ambao wamekuwa wakifanya wanasheria na kuingilia kesi za watu wakidai wanawasaidia.

“Lakini naomba mkatusaidie kuwaangalia pia wale wanaojifanya ni wanasheria kwa kigezo cha utaalamu wa kuongea . Kuna baadhi ya wazee waliopo katika maeneo yenu ambao wao sasa wameibuka kuwa vishoka wa sheria,wamekuwa wakiingilia kesi za watu na kujifanya wao ni ndugu matokeo yake wamekuwa wakiwaomba fedha ili kuwasaidia kushughulikia kesi zao”,alieleza Tarimo.

Alisema watu hao wamekuwa wakiwapotezea watu muda wa kupata haki zao,wanawaingiza katika umaskini kwa sababu wanachukua fedha kutoka kwao hivyo kuwaomba wasaidizi wa kisheria na jamii kwa ujumla kutoa elimu kwa wananchi watumie wasaidizi wa kisheria ambao wanatoa huduma bure.

Alieleza kuwa hivi sasa kuna kesi nyingi kuhusu wanawake waliofiwa na waume zao ‘wajane’ wanapata changamoto ya mali,migogoro ya ardhi. "Waelekezeni waende kwenye mabaraza ya kata badala ya kuwapotezea muda kwa kupeleka kusikohusika,msiluhishe kesi za ubakaji,ulawiti na pindi msaidizi wa kisheria unapoletewa kesi ukashindwa kujua ufanyeje basi wasiliana na Mwanasheria wa halmashauri yako akushauri namna ya kufanya kwa kile ulicholetewa na mteja wako",alifafanua.

“Wasaidizi wa Kisheria sasa wameingizwa katika kamati za MTAKUWWA ili kuongeza nguvu katika mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Shirikianeni na watendaji wetu kutoa taarifa za matukio ya ulawiti na ubakaji ili hatua zichukuliwe kukomesha matukio ya ukatili. Naomba tufanye kazi katika hali ya uaminifu na uadilifu,tutende na tuenende katika haki”,alisema.

“Napenda kutoa shukrani zetu za dhati mkoa wa Shinyanga kwa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kuwa msaada mkubwa katika mkoa wa Shinyanga. Mikoa ni mingi lakini wameona waje kwetu kutuongezea nguvu na tunazidi kuwaomba wakaribie zaidi Shinyanga",aliongeza Tarimo.

Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESHI la Shinyanga mjini  alisema la mafunzo hayo yaliyowezeshwa na TGNP ni kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 60 kutoka halmashauri ya Kishapu, Ushetu, Msalala na Kahama Mji yaliyolenga kuwajengea uwezo namna ya kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia.

Alisema mpaka sasa katika mkoa wa Shinyanga kuna jumla ya  Wasaidizi wa Kisheria 174 wasaidizi wa kisheria ambao wataongeza nguvu katika kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia yakiwemo ya ubakaji,ulawiti,vipigo,migogoro ya ndoa,mirathi,ardhi na mimba na ndoa za utotoni.

Akitoa neno la shukrani, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Richard Julius kutoka kijiji cha Busongo kata ya Mwamashele wilayani Kishapu alisema watakwenda kutekeleza yote waliyofundishwa na kuepuka kuwa vishoka kwa kujifanya wanasheria kwao wao ni wasaidizi wa kisheria tu na kwamba wataenda  kusaidia wananchi wanaosumbuka katika jamii.

Miongoni mwa mada zilizofundishwa na kujadiliwa wakati wa mafunzo hayo ya siku 6 ni pamoja na masuala ya Ndoa,mirathi,MTAKUWWA na majukumu ya wasaidizi wa kisheria ikiwemo namna ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Jamii.

Katika mafunzo hayo Wasaidizi wa Kisheri wamejiwekea malengo mbalimbali katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii ikiwa ni pamoja na kujenga mahusiano ya kazi na viongozi kwa kujitambulisha katika kamati za MTAKUWWA.

Malengo mengine ni kupunguza ukatili wa kijinsia katika jamii kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano na vikundi,shuleni,nyumba za ibada,kutoa taarifa haraka kwenye vyombo vya dola na kuhamasisha utungaji wa sheria ndogo ndogo zinazozingatia usawa wa kijinsia kwa kufanya uchambuzi wa mila nzuri na potofu/kandamizi, kufanya uchechemuzi na kukutana na viongozi wa halmashauri za vijiji na mitaa.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia leo Jumanne Oktoba 6,2020 katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel Mjini Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia leo Jumanne Oktoba 6,2020 katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel Mjini Shinyanga. Kulia ni Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria halmashauri ya wilaya ya Kishapu Efrem Kilango, kushoto ni Mwezeshaji katika Mafunzo hayo, Wakili Neema Ahmed.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia. Wa kwanza kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Mwanasheria Jenesia Mavere na Wakili Neema Ahmed ambaye pia ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo. Wa kwanza kulia ni Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESHI la Shinyanga mjini akifuatiwa na Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria halmashauri ya wilaya ya Kishapu Efrem Kilango.
Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESHI la Shinyanga mjini akizungumza wakati mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia yakifungwa.
Mwezeshaji wa Mafunzo, Wakili Neema Ahmed akizungumza wakati mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia yakifungwa. Kushoto ni Mwezeshaji Msaidizi wa Mafunzo hayo, Mwanasheria Jenesia Mavere, kulia ni Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Richard Julius kutoka kijiji cha Busongo kata ya Mwamashele wilayani Kishapu akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Wasaidizi wa Kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Kishapu/ Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), wilaya ya Kishapu, Mwajuma Abeid akiwasihi Wasaidizi wa kisheria kushirikiana na ofisi ya Ustawi wa Jamii wilaya na kwamba atawajulisha wajumbe wa MTAKUWWA kuwa sasa Paralegals wameingia kwenye kamati za MTAKUWA kama wajumbe.
Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria halmashauri ya wilaya ya Kishapu Efrem Kilango akiwakumbusha wasaidizi wa kisheria kutimiza wajibu wao kwa kusaidia jamii hususani watu wa hali ya chini/watu duni,tufanye yaliyo mema kwa kuzingatia taratibu zote mkaache alama njema kwa jamii.

"Tunawashukuru wadau TGNP kwa kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria, mnasaidiana vizuri na serikali kuwafikia wananchi",alisema Kilango. 
Msaidizi wa Kisheria Buyamba Ngogeja kutoka Kishapu akiongoza mjadala wa kutengeneza Mpango Kazi wa Wasaidizi wa Kisheria waliopata mafunzo ya namna ya kupambana na Ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mwezeshaji katika Mafunzo hayo, Wakili Neema Ahmed akizungumza ukumbini
Mwezeshaji katika Mafunzo hayo, Wakili Neema Ahmed akizungumza ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akipiga picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia leo Jumanne Oktoba 6,2020 katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel Mjini Shinyanga.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo akipiga picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria mkoa wa Shinyanga kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia leo Jumanne Oktoba 6,2020 katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel Mjini Shinyanga.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com