Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHUNI WASAMBAZA PICHA ZA MGOMBEA WA NCCR -MAGEUZI ZIKIONESHA ANAGOMBEA KUPITIA CCM NGOKOLO - SHINYANGA MJINI


Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geoffrey Mwangulumbi akionyesha vipeperushi vilivyosambazwa kinyume na taratibu vikimuonyesha mgombea wa NCCR Mageuzi akiwa kwenye vipeperushi vya CCM. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Vipeperushi vyenye picha ya mgombea udiwani Kata ya Ngokolo kwa tiketi ya NCCR -Mageuzi, Charles Shigino vikimuonesha ndiye mgombea wa kata hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mgombea Udiwani kata ya Ngokolo kupitia Chama Cha NCCR - Mageuzi Charles Shigino akionyesha vipeperushi hivyo ambavyo vinamuonyesha kuwa yeye ni mgombea wa CCM
Mgombea wa CCM Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu akizungumzia sakata hilo.
***
Na Damian Masyenene -Shinyanga
KAMATI ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini leo Oktoba 16, 2020 imekutana kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na Mgombea Udiwani Kata ya Ngokolo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Victor Mkwizu dhidi ya mgombea wa NCCR - Mageuzi, Charles Shigino juu ya usambazaji wa vipeperushi vyenye picha ya Charles Shigino vikionyesha ndiye mgombea wa CCM.

Akitangaza uamuzi wa kamati hiyo leo katika ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Msimamizi wa Jimbo hilo, Geoffrey Mwangulumbi amesema kuwa kamati hiyo ilipokea malalamiko leo asubuhi kutoka CCM wakilalamikia uwepo wa vipeperushi vinavyosambazwa kinyume na utaratibu vikimtangaza Charles Shigino kuwa ndiye mgombea wa chama hicho kata ya Ngokolo badala ya Victor Mkwizu, huku vipeperushi hivyo vikiwa havijathibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mwangulumbi ameeleza kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo walikutana na kumuita mgombea anayeonekana kwenye vipeperushi hivyo (Shigino), ambaye baada ya kuhojiwa alikana kuvitambua vipeperushi hivyo.

"Tume inakemea vikali tabia hii kwa vyama vyote visijaribu kutumia majina na alama (nembo) za vyama vingine kujinadi na kutafuta umaarufu, hili ni kosa la jinai," amesema Mwangulumbi.

Katika hatua nyingine, Mwangulumbi amesema hatua hiyo inavikaribisha vyombo vya usalama kulishughulikia kwa kufuatilia na kubaini waliosambaza vipeperushi hivyo na walivisambaza kwa nia gani.

"Yeyote atakayekutwa na vipeperushi hivi, ama steshenari itakayokutwa inaviandaa watachukuliwa kwamba ndiyo wanahusika kuvisambaza, tunatoa maelekezo kwa wagombea kukanusha hadharani kutohusika kwao na jambo hili," amesema.

Akizungumzia jambo hilo, Mgombea Udiwani wa Kata ya Ngokolo kupitia NCCR Mageuzi, Charles Shigino ambaye pia ni Mgombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia chama hicho amesema mtindo uliotumika kumchafua na kuleta mkanganyiko ni matokeo ya uwezo mdogo wa wanasiasa kushindana kwa hoja.

"Nimeshangaa sana kuona picha zangu zikionesha kuwa mimi ni mgombea kupitia CCMM,wakati mimi nipo NCCR - Mageuzi, kitendo hiki kinachanganya wananchi. Picha hizi zimenikwaza, kuninyong'onyesha na kunidhalilisha kwa sababu hizo ni picha za mwaka 2012 wakati niko CCM kwenye kura za maoni, wamefanya wapiga kura washindwe kuelewa",amesema Shigino.

"Hiki kitendo cha kusambaza picha zangu ni cha kihuni Lazima nikutane na vyombo vya ulinzi na usalama tuweze kubaini waliofanya uhuni huu, nawaomba wananchi wapuuze uzushi huu unaotengenezwa na wanasiasa uchwara," amesema Shigino.

 Kwa upande wake Mgombea Udiwani kata ya Ngokolo, kupitia CCM, Victor Mkwizu ameeleza kusikitishwa na kitendo hicho akibainisha kuwa hizo ni mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com