Na Mwandishi Wetu DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi, Simba SC wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Kwa ushindi huo, Wekundu hao wa Msimbazi wanafikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi tano, sasa wakiwazidi wastani wa mabao tu mahasimu wao, Yanga SC wanaofuatia nafasi ya pili.
Mechi ya watani wa jadi, baina ya miamba hiyo miwili ya soka Tanzania, Simba na Yanga utakaopigwa Oktoba 18 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam ndiyo utaamua timu ya kukaa kileleni wiki mbili zijazo.
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hance Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Joseph Masiga wa Mwanza na Geoffrey Msakila wa Geita, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0 na yote yakifungwa na wachezaji wa kigeni.
Alianza mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda na mfungaji Bora wa Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo iliyopita, Meddie Kagere kufunga la kwanza dakka ya tat utu akimaliza kazi nzuri ya kiungo Mzamba, Rally Bwalya.
Akafuatia mshambuliaji mpya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Chris Mushimba Kope Mugalu kufunga la pili dakika ya tano tu akimalizia pasi ya kiungo kutoka Msumbiji, LuÃs Jose Miquissone.
Na kabla ya kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza, Kagere mshambuliaji wa zamani wa ES Zarzis ys Tunisia na KF Tirana ya Albania akafunga bao lake la pili leo na la tatu kwa Simba SC dakika ya 40 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Kipindi cha pili kiungo wa zamani wa Mamelodi Sundowns, Chippa United na Royal Eagles za Afrika Kusini, Luis Jose Miquissone akakamilisha shangwe za mabao kwa kuifungia Simba SC bao la nne dakika ya 54.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Kelvin Friday dakika ya tisa limewapa ushindi wa 1-0 wenyeji, Biashara United dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Mchezo kati ya Azam FC na Kagera Sugar unafuatia Saa 1:00 usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Na Raundi ya tano itahitimishwa kesho kwa mchezo mmoja, kati ya KMC na Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha JKT Tanzania kilikuwa; Patrick Muntary, Michael Aidan, Nurdin Mohamed, Frank Nchimbi, Edson Katanga, Richard Maranya/Daniel Lyanga dk58, Mgandila Shaaban/Kelvin Nashon dk61, Daniel Mecha, Kelvin Sabato, Adam Adam na Mwinyi Kazimoto.
Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussien ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone/Hassan Dilunga dk77, Rally Bwalya, Meddie Kagere/Muzamil Yassin dk59, Chriss Mugalu na Clatous Chama/Bernard Morrison dk73.
CHANZO - BINZUBEIRY BLOG
Social Plugin