Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MABINGWA WATETEZI SIMBA SC WAPIGWA TENA....RUVU SHOOTING YATAMBA....MTIBWA SUGAR NAO WAICHAPA AZAM FC


MABINGWA watetezi, Simba SC wamepoteza mechi ya pili mfululizo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa 1-0 na Ruvu Shooting iliyomaliza pungufu ya mchezaji mmoja jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanaifanya Ruvu ifikishe pointi 12 baada ya kucheza mechi nane na kusogea nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya timu 18, wakati Simba iliyofungwa 1-0 pia na Tanzania Prisons kwenye mechi iliyopita Sumbawanga, inaangukia nafasi ya nne ikibaki na pointi zake 13 baada ya mechi saba.

Azam FC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 21 bada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wenye pointi 19 za mechi saba. 

Bao lililozamisha Simba SC leo, mabingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo – limefungwa na Nahodha wa Ruvu Shooting, Fully Zulu Maganga aliyenufaika na makosa ya beki Muivory Coast, Serge Pascal Wawa aliyepiga fyongo na mpira kumkuta mfungaji aliyemchambua kipa Beno Kakolanya dakika ya 36.

Ruvu Shooting inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Tanzania na klabu ya Yanga miaka ya 1980, Charles Boniphace Mkwasa ilimaliza pungufu baada ya mchezaji wake Shaaban Msala kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75.

Lakini Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven-Ludwig Vandenbroeck ilishindwa kutumia fursa hiyo japo kupata bao la kusawazisha licha ya kupewa hadi penalti, ambayo Nahodha John Raphael Bocco aligongesha mwamba na mpira ukarudi uwanjani dakika ya 79.

Refa Abdalah Mwinyimkuu wa Singida alitoa penalti hiyo baada ya beki wa Ruvu Shooting, Renatus Ambroce Kisase kuinua mguu kuondosha mpira kwenye boksi lao mbele ya kiungo wa Simba SC kutoka Msumbiji, Luis Miquissone. 

Refa Mwinyimkuu aliyekuwa anasaidiwa na Abdulaziz ally wa Arusha na Josephat Kasilirwa wa Iringa, alirefushwa mchezo kwa dakika sita zaidi ili kufidia muda uliopotezwa kwa matukio mbalimbali nab ado Ruvu Shooting wakafanikiwa kulinda ‘bao lao la dhahabu. 

Mechi nyingine za Ligi Kuu, bao pekee la Jaffar Salum Kibaya dakika ya 62 lilitosha kuipa Mtibwa Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.

Nayo Tanzania Prisons ikaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC bao pekee la Ramadhani Ibata dakika ya 88 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk57, Ibrahim Ajibu, Rally Bwalya/John Bocco dk66 na Francis Kahata/Bernard Morrison dk46.

Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Santos Mazengo, Renatus Ambroce, Juma Nyosso, Zuberi Dabi, Mohammed Issa/Renatus Kisase dk70, Abraham Mussa, Shaaban Msala, Fully Zulu Maganga/Graham Naftar dk70, David Richard na Emmanuel Martin.

CHANZO - BINZUBEIRY BLOG


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com