Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack amesema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28,2020 unakuwa salama huku akiwaonya baadhi
ya watu wanaopanga kufanya vurugu kuachana na mipango hiyo.
Telack ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Shinyanga ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 24,2020 wakati akizungumza na vyombo vya
habari ofisini kwake ambapo pia amewatahadharisha vijana kuepuka kutumiwa na wanasiasa
kuharibu amani ya nchi.
“Ninawaomba
sana wananchi wa mkoa wa Shinyanga wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze kwenda
kupiga kura Oktoba 28,2020 ili wachague viongozi wale wanaona wanaweza
kuendesha nchi yetu.
Muda wa
kupiga kura utaanza saa moja asubuhi mpaka saa 10 jioni,niwasihi wananchi
wawahi kwenye vituo vya kupigia kura ili kuepuka msongamano usio wa lazima.
Baada ya kupiga kura wananchi warudi majumbani wakaendelee na shughuli zao kama
kawaida”,amesema Telack.
“Niwasihi
sana vijana wetu wasitumike kujaribu kuharibu amani yetu kwa namna
yoyote,tupige kura turudi majumbani mwetu kuendelea na shughuli zingine,
matokeo yatatangazwa na Tume ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria .Kila kituo
kitakuwa na Mawakala wa vyama vya siasa hivyo hakuna atakayeiba kura, achaneni
na mambo ya kusema mnakaa vituoni kulinda kura. ”,ameongeza Telack
Mkuu huyo wa
mkoa amesema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba watu wote wanaotaka
kwenda kupiga kura,wanapiga kura na shughuli zote za kijamii zinaendelea bila
kuathiriwa na kitu chochote.
“Naomba
kuwahakikishia wananchi wote wa Shinyanga kuwa usalama utakuwepo wa kutosha kwa
hiyo asiwepo mtu yeyote ambaye atajaribu kwa namna yoyote kuzuia wananchi
wasiende kupiga kura. Wewe ukiona mtu anazunguka barabarani anajaribu kukuzuia
wala usirudi nyuma kwa sababu usalama utakuwepo wa kutosha”, ameeleza Mkuu huyo
wa mkoa.
Amewasihi wale
wote wanaodhani wamejiandaa kufanya fujo yoyote siku ya uchaguzi waache kwa
sababu serikali imejiandaa vizuri kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama.
“Napenda kuwafahamisha kuwa yapo maisha baada ya uchaguzi, Hii Tanzania ni ya kwetu,tuilinde kwa nguvu zetu zote na tusijaribu na asijaribu mtu yeyote kufanya vitendo vya uvunjivu wa amani”,amesema.
Katika hatua
nyingine amevitaka Vyombo vya habari na waandishi wa habari kutotangaza matokeo
ya uchaguzi akidai kuwa wenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi ni Tume
ya Taifa ya Uchaguzi.
“Waandishi
wa habari msitangaze matokeo ya uchaguzi kwa mhemko wowote. Sasa usianze sijui
watu wanajumlisha matokeo ya kata na wewe unaanza kutoa matokeo, Hapana. Kuweni Neutral kwenye jambo hili la
uchaguzi. Msikubali kutumika ili thamani ya kazi zenu iendelee kubaki kwani
kuna maisha baada ya uchaguzi”,amesema Telack.
Kwa upande
wake, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga amesema maandalizi
ya uchaguzi yamekamilika na kwamba jumla ya vituo vya kupigia kura mkoani
Shinyanga vitakuwa 2700.
Social Plugin