PWANI WAADHIMISHA SIKU YA USHAIRI WA WATOTO DUNIANI 'WoChiPoDa'


WAKATI siku ya Ushairi wa Watoto 'World Children’s Poetry Day- - WoChiPoDa'  ikiadhimishwa katika maeneo mbalimbali duniani kote, wazazi, walezi na walimu nchini wameaswa kuwapa fursa watoto wao ya kushiriki katika mafunzo na matamasha ya uandishi wa ushairi na usomaji vitabu ili kuwajengea uwezo wa kuandika maandiko mbalimbali kulingana na mazingira wanayoishi kwani kufanya hivyo kutasaidia kuibua na kuendeleza vipaji vyao katika kuliletea taifa maendeleo kwa siku za baadaye.

Hayo yalisemwa na Mratibu wa siku ya ushairi WoChiPoDa mkoa wa Pwani Bi. Rehema  Kawambwa alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya ushairi wa watoto duniani yanayofanyika Jumamosi ya kwanza ya mwezi Oktoba, ambayo mwaka huu yalifanyika katika shule ya msingi Kiluvya ‘B’ Kisarawe mkoani Pwani.

Rehema alisema ili kujenga uelewa kwa watoto kulingana na mazingira wanayoishi ni wazi kuwa ipo haja ya kila mzazi kutambua kuwa watoto wanayo haki ya kushiriki katika matamasha kama hayo ambayo yatawajengea uwezo wa kuwa waandishi wa ushairi na insha na vitabu mbalimbali vya hadithi na hatimae kuwa sehemu muhimu ya kuielimisha jamii ya Watanzania.

Alisema kazi ya uandishi ni kazi kama kazi zinginine hivyo endapo mtoto ataandaliwa vizuri na kuwa mwandishi mzuri si tu atakua sehemu ya kuwaelimisha wengine lakini pia ujuzi na kipaji alichonacho kitamsaidia kujiingizia kipato kama ilivyo kwa waandishi wengine wenye majina makubwa kote ulimwenguni.

"Ushiriki wa watoto wetu katika matamasha kama haya yanatoa fursa ya kuwajenga na kuwapata washairi wengi kwani ikizingatiwa hivi sasa hamasa ya kusoma vitabu imeshuka hivyo kwa hatua hiyo itasaidia kupata taifa lenye watu wanaopenda kusoma vitabu kwa siku za usoni’’,alisema Rehema.

"Pia, niende mbali zaidi uandishi wa ushairi pia utamuongezea mtoto kuendana na mazingira halisi hivyo kuandika mashairi kutamsaidia pia kuandika vitabu ambavyo faida zake kwa baadae ni kuviingiza sokoni ili kuwanufaisha kibiashara hivyo ni jukumu la wazazi kujitoa kwa kila hali ili kuwapa nafasi ya kujiinua kiuchumi kupitia uandishi’’,alisema.

Naye mdau wa elimu ambae pia ni mzee maarufu katika kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe Mohammed Pweku alisema ili kupata taifa zuri kwa siku za baadae ipo haja ya wazazi kutumia fursa mbalimbali za kielimu ambazo zimekuwa zikijitokeza ili kuwaimarisha zaidi badala ya kuwanyima nafasi hizo na hivyo kupelekea kujiingiza katika matukio yasiyofaa.

"Alisema kutokana na watoto wengi kuharibika kimaadili ni wakati wao sasa wazazi tukatumia nafasi hizi zinazotolewa na wadau wa elimu katika kuwahamasisha na kuwashinikiza watoto kushiriki ili kuondokana na tabia ya kushinda shinda mitaani hususani katika siku za mapumziko ili kuwaepusha watoto wetu na makundi yakatayochangia kumomonyoka kwa maadili’’.

Wakizungumza kwa niaba ya watoto walioshiriki katika tamasha hilo wanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kiluvya ‘B’ Abdallah Mbonde na Noela Urasa walisema kuwa kupitia tamasha hilo kutawafanya kupanuka kimawazo kwani ikizingatia hivi sasa Taifa limejikita katika ukuaji wa Tanzania ya viwanda hivyo uandishi wa vitabu vya ushairi utawawezesha kuendeleza vipaji vyao lakini pia kama chanzo cha biashara kwani kupitia viwanda vya uchapishaji ili kuliendeleza taifa.

Siku ya ushairi wa watoto duniani ilianzishwa mnamo mwaka 2014 na Bi. Gloria Gonsalves aishie nchini Ujerumani ambaye pia ni mwandishi wa vitabu na mashairi ikiwa na lengo la kuinua vipaji vya watoto kuwaweka pamoja na kwa kuwapa motisha ya kupenda na kujifunza uandishi wa mashairi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post