WATANO MBARONI VURUGU ZA WAFUASI WA WAGOMBEA UBUNGE CCM NA CHADEMA SHINYANGA MJINI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kujeruhi na kuharibu mali baada ya kutokea vurugu kati ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiandamana na wagombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini wa CCM  (Patrobas Katambi) na CHADEMA (Salome Makamba)  wakitoka kwenye mikutano ya Kampeni za Uchaguzi wakielekea kwenye ofisi za vyama vyao. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba vurugu hizo zimetokea jana Jumamosi Oktoba 24,2020 majira ya saa moja jioni. 

“Tukio hilo limetokea wakati wagombea wa nafasi ya ubunge jimbo la shinyanga mjini wa CCM na CHADEMA Shinyanga mjini wakiwa wanarudi kutoka kwenye maeneo ya kampeni zao wakielekea katika ofisi zao za vyama vya siasa walikutana katika eneo la Japanise Corner na vurugu zikaanza katika eneo hilo”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

“Vurugu hizo zilipelekea Hasani Tito Masanja (28), mkazi wa Majengo kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali kidevuni akiwa na gari alilokuwa anaendesha lenye namba za usajili T. 786 BEK TOYOTA NOAH, gari ya matangazo ya mgombea ubunge CCM nalo lilivunjwa vioo vyote, pia Doto Samweli Joshua (29), mkazi wa Lubaga alivunjiwa kioo cha gari cha mbele gafi ikiwa na namba za usajili T. 444 CFA SUZUKI SWIFT, na pia Secilia Sangaluka, (42), alivunjiwa taa Indicator ya nyuma kushoto”, amesema Kamanda Magiligimba. 

Amesema Jeshi la polisi linawashilikilia watuhumiwa watano ambao ni Ramadhan Mohammed, (20), na mkazi wa Ndembezi, Yuda Kanoku, (22), mkazi wa Ibadakuli, Frank Chiza, (20), mkazi wa Kahama, Timoth Amos (20), mkazi wa Ibadakuli na Mussa Luhende, (21), mkazi wa ibadakuli ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujeruhi na kuharibu mali. 

Kamanda Magiligimba amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. 

Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wanasiasa pamoja na wafuasi wao kuacha kufanya siasa za vurugu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na wafanye kampeni zao kwa amani na utulivu na mara baada ya mikutano kumalizika wananchi wanatakiwa kutawanyika na siyo kufanya maandamano kuelekea kokote kule.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post