Kikundi cha Sanaa cha Shinyanga Arts Group Kikitumbuiza katika halfa ya ufunguzi wa Maonesho ya Vikundi vya Sanaa vinavyotoa elimu ya Maadili kwa njia ya Sanaa yaliyofanyika Mjini Shinyanga. Picha na Salvatory Ntandu
Kikundi cha Sanaa cha Shinyanga Arts Group Kikitumbuiza katika halfa ya ufunguzi wa Maonesho ya Vikundi vya Sanaa vinavyotoa elimu ya Maadili kwa njia ya Sanaa yaliyofanyika Mjini Shinyanga.
Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Beda Chamatata, akizungumza na Wasanii (hawapo pichani) katika ufunguzi Maonesho ya Vikundi vya Sanaa vinavyotoa elimu ya Maadili kwa njia ya Sanaa yaliyofanyika Mjini Shinyanga.
Katibu Msaidizi ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Magharibi Gerald Mwaitebele akizungumza na wasanii wa mbalimbali mkoani Shinyanga(Hawapo Pichani)
*****
Na Salvatory Ntandu - Shinyanga
Wasanii Mkoani Shinyanga wametakiwa kutunga nyimbo zenye Ujumbe na Maudhui ya kuifundisha jamii kuhusiana na Maadili kupitia sanaa mbalimbali wanazozifanya ili kutokomeza vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa ngazi mbalimbali unaosababisha uwepo migongano ya kimaslahi.
Kauli hiyo imelewa leo na Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Beda Chamatata, katika hafla ya Uzinduzi wa Maonesho ya Vikundi vya Sanaa vinavyotoa elimu ya Maadili kwa njia ya Sanaa yaliyofanyika Mjini Shinyanga.
Alisema kuwa Wasanii wanapaswa kubadilika kwa kutunga nyimbo,maigizo,mashairi yenye ujumbe wa kuwakumbusha viongozi kuhusiana na Maadili na athari zake pindi viongozi wanapokengeuka ili waweze kubadilika na kuachana na vitendo ambavyo vinamadhara makubwa katika jamii.
“Wasanii ni kioo cha Jamii hebu tusaidieni kufikisha ujumbe kwa Jamii kuhusiana na elimu hii ya Maadili ili kuwasaidia wananchi kuwafichua viongozi wa umma ambao wanakiuka viapo vyao na kuanza kutumia ofisi za Umma kwa maslahi yao binafsi,”alisema Chamatata.
Aliongeza kuwa Wasanii wanapaswa kubadilika na kuwa wabunifu katika kazi wanazozitekeleza ili ziweze kuleta tija kwao na kwa jamii ambayo wanaihudumia kwa kutumia sanaa wanazozitekeleza sambamba na kuwakumbusha kuhusiana na suala la Uzingatiaji wa maadili kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi.
Kwa Upande wake Katibu Msaidizi ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Gerald Mwaitebele alisema wameamua kuwatumia wasanii kuwa Mabalozi wa kufika ujumbe kwa jamii kwani kupitia kazi za sanaa wanazozitekeleza ili kufikka ujumbe Mahususi kwa wakati na kwa lugha inayoelewaka kuhusiana na Umuhimu wa uzingatiaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Ofisi ya Rais ,Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Magharibi leo tumepata mabalozi wapya ambao ni wasanii kupitia elimu tuliyowapatia ya maadili,tunaamini watatunga nyimbo zenye ujumbe wa kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia maadili ya viongozi wa Umma,”alisema Mwaitebele.
Naye Ofisa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga Janeth Mompome amewataka Wasanii wote mkoani humo kusajili vikundi vyao ili viweze kutambulika kisheria sambamba na kurasimisha kazi zao ili kuepuka usumbufu unajitokeza pindi wanapopata nafasi za kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.
“Mkoa wa Shinyanga unavikundi vya Sanaa zaidi ya 36 ambavyo vimesajiliwa kisheria huku kunavingine havijasajiliwa na vinaendelea kufanya kazi niwaagize viongozi wa vikundi hivi wafike katika ofisi za utamaduni wakasajili haraka kwa sababu ghama zake haizidi 45,000 tu,”alisema Mompome.
Vikundi vitatu vya vilivyopatiwa mafunzo na Ofisi ya Maadili Kanda ya Maharibi ni pamoja na Shinyanga Arts group,Viwawashi Arts group na Jambo arts group.
Social Plugin