Watu watano wamefariki dunia na wengine 10 wamejeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani iliyohusisha daladala na lori la mchanga katika eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam iliyotokea alfajiri ya leo Jumatatu, Oktoba 5, 2020.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Aidha, akielezea chanzo cha ajali hiyo iliyotokea saa 10 alfajiri leo, Mambosasa amesema dereva wa daladala alipita wakati taa nyekundu (zinazomzuia kupita) zikiwa zimewaka.
Daladala hiyo hufanya safari zake kati ya Temeke na Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni daladala iliyopata ajali Chang'ombe na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe.
DC Gondwe amesema mpaka sasa dereva hajulikani alipo kwani mara baada ya ajali hiyo alitoweka kusikojulikana.
"Niwape pole familia ambazo wamepoteza wapendwa wao, ambapo mpaka sasa hivi wamefariki 5 na majeruhi 10, inaonekana ni uzembe wa madereva maana wakati wanatoka Buza abiria walikuwa wanamuambia apunguze mwendo na alipofika kwenye mataa taa nyekundu ilikua imewaka, abiria wakamkumbusha lakini akawaambiwa wasimfundishe kazi", amesema DC Gondwe.
Aidha Gondwe ameongeza kuwa, "Dereva yeye kakimbia na serikali ina mkono mrefu tutamfikia, nitoe wito kwa madereva wa dalaladala wamebeba uhai wa watu, mali zinatafutwa, uhai wa mtu ukipotea hauwezi kurejea kwa hiyo wafuate sheria ili kuokoa maisha"
Social Plugin