Askofu wa kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania ( IEAGT) David Mabushi akihubiri neno la utangulizi kabla ya kuanza maombi katika ibada ya kuombea uchaguzi mkuu Tanzania uwe wa amani.
Na Suzy Luhende - Shinyanga
ASKOFU wa Kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania ( IEAGT) David Mabushi ameongoza maombi maalumu ya siku tatu ya kuombea uchaguzi mkuu wa Tanzania ili uwe wa amani na utulivu.
Akihubiri neno la Mungu la utangulizi kabla ya maombi leo, Askofu Mabushi katika kanisa hilo lililoko kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga ,amesema ameamua kufanya maombi na waumini wa kanisa hilo ili kuombea uchaguzi wa Tanzania uweze kuwa wa amani kwa sababu maombi ya kanisa yana nguvu ya kipekee.
Askofu Mabushi amesema maombi ya kanisa yana nguvu, pia yana majibu na matokeo ya kipekee sana ikiwa kanisa litasimama kwa jukumu hilo kikamilifu bila kuzembea.
"Kanisa likizembea kuomba matokeo mabaya yanapata nafasi na hatimaye ni huzuni na mateso vinatokea , hivyo kanisa la Mungu halipaswi kuzembea linatakiwa kuomba mapema ili kuzuia mabaya yasitokee katika jamii na kuharibu mfumo wa maisha",amesema Askofu Mabushi.
Amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi ni muhimu kanisa likafanya maombi ili kuzuia hali ya uvunjifu wa amani kwa Taifa la Tanzania katika zoezi la uchaguzi mkuu.
"Soma Matendo 12:1-5, Yeremia 30:12-15, na Mwanzo 20:17-18 utaona Herode alifanya vita na Kanisa alimuua Yakobo kwa kuwa kanisa halikuchukua hatua ya haraka ya kufanya maombi,lakini alipotaka kumuuwa Petro kanisa lilifanya maombi na Petro alikwepa kifo kwa sababu ya maombi yalizuia",amesema Askofu Mabushi.
Aidha amesema baada ya kutokea ugonjwa wa Virus vya Corona (Covid 19) kanisa lilichukua nafasi mapema na kufanya maombi ya vita, ugonjwa huo haukuendelea kuwepo katika nchi ya Tanzania kwa sababu kanisa lilisimama imara katika maombi, halikuteteleka.
Pia amesema makanisa yote yakishirikiana kwa maombi uchaguzi utakuwa ni wa amani na utulivu kinachotakiwa ni kuomba kwa kudhamiria na kuachana na mazoea na kuzembea.
Maombi ya kanisa yana nguvu kuliko maombi ya mtu mmoja mmoja, hivyo katika wakati huu wa uchaguzi ni vizuri makanisa yakamlilia Mungu ili aweze kuonekana na kuweza kuchagua kiongozi mwaminifu mwenye hekima na busara na mpenda maendeleo.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo Estomine Henry na Elizabeth Jackob wamesema watu wote wakiomba katika roho na kweli Mungu atasimama na amani itatawala, hivyo ni vizuri makanisa yote na dini zote zikashikamana kuliombea Taifa ili uchaguzi wa madiwani, ubunge na Urais ukawa wa amani.
Askofu wa kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania ( IEAGT) David Mabushi akihubiri neno la utangulizi kabla ya kuanza maombi katika ibada ya maombi iliyofanyika kanisani hapo.
Sehemu ya Waumini wa kanisa hilo wakimsikiliza Askofu David Mabushi akihubiri katika ibada ya maombi kanisani hapo.
Social Plugin