Mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Bernard Membe amesisitiza kuwa bado ni mgombea wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Membe aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 amesema hayo leo Jumatatu tarehe 19 Oktoba 2020 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mwanadiplomasia huyo amejitokeza kuzungumza na waandishi wa habari akiwa na mgombea wake mwenza, Profesa Omar Fakh zikiwa zimesalia siku tisa kufikia Uchaguzi Mkuu.
Tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi Agosti 26, 2020, Membe amefanya mikutano mitatu katika mikoa ya Pwani na Lindi na baadaye hapo akasafiri kwenda Dubai kuhudhuria mkutano na uchunguzi wa afya yake, tangu aliporejea Tanzania amekuwa kimya.
Membe amenza kuzungumza kwa kusema, “Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa.”
Amesema, ukimya wake wa muda wa kutoonekana majukwaani alikuwa anafanya mikakati ya chini kwa chini na sasa umewadiwa muda wa kurejea kufanya kampeni alizoziita za kimbunga.
Kauli ya Membe imekuja wakati Ijumaa Oktoba 16, 2020 Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.
Mbali na Zitto, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika urais. Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.
“Nataka kufunga bao dakika ya 89 kutoka benchi. Watanzania mkae macho na mkae chonjo. Tumefanya kazi huku chini sasa tunakuja juu kupata bao la ushindi dakika 89 na dakika za nyongeza,”- Amesema
Social Plugin