Bil 5.26/- zatumika kujenga barabara Ngara


 SHILINGI bilioni 5.26 zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi na  matengenezo ya barabara katika wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

“Kati ya hizo, shilingi bilioni 1.1 zimetengeneza barabara kwa kiwango cha lami kilomita 4.5 katika makao makuu ya wilaya hii.”

Hayo yamesemwa jana (Jumatano, Septemba 30, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Rulenge, katika mikutano uliofanyika kwenye stendi ya Rulenge.

Amesema kiasi kingine cha shilingi bilioni 4.16 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwemo barabara za Muhweza – Mukarehe, Keza – Nyanzovu, Mukalinzi – Mulonzi, Kibuba – Gwenzaza, Murugwanza – Runzenze (Airstrip), Chivu – Ntobeye – Nyakiziba, Buhororo – Mukididili, Ngara – Kumutana na Buhororo – Ruganzo (Airstrip)

Mheshimiwa Majaliwa ambaye leo anamalizia ziara yake mkoani Kagera ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ngara, Bw. Ndayisaba George Ruhoro na mgombea udiwani wa CCM wa kata ya Rulenge, Bw. John Niyonzima.

Mapema, akiwa njiani kuelekea Ngara akitokea Bukoba mjini, Mheshimiwa Majaliwa alisimamishwa na wakazi wa kata za Nyaishozi (Karagwe) na Kasulo Benaco (Ngara) ambako pia aliwanadi madiwani wa kata hizo. Pia aliwaeleza kwamba barabara ya kutoka Omurushaka hadi Benaco itajengwa kwa kiwango cha lami.

“Kwenye Ilani ya uchaguzi iliyopita ambayo inaisha sasa, barabara hii ilielezwa kwamba itakamilishwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, na sasa inaenda kujengwa kwa lami kwa sababu kazi imeshafanyika.”

Pia aliitaja barabara nyingine ya kutoka Bugene – Kasulo (BENACO) yenye urefu wa km. 124 ambayo inatajwa kwenye uk. 75 wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwamba ni miongoni mwa barabara zitakazoanza kujengwa upya kwa kiwango cha lami.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post