BWENI LA SHULE YA SEKONDARI UCHIRA ISLAMIC LATEKETEA KWA MOTO


Bweni la Shule ya Sekondari ya wasichana ya Uchira Islamic iliyoko wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, limeteketea kwa moto jioni ya Oktoba 16, 2020, huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana mpaka sasa na hakuna kifo wala madhara kwa mwanafunzi yeyote.

Inspekta Abraham Ntezidyo, kutoka Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Kilimanjaro, amesema  taarifa za moto huo walizipata jana jioni majira ya saa 12:00 na moto umeteketeza jumla ya vitanda 25 ambavyo walikuwa wakilalia wanafunzi 50.

“Athari kubwa ni kwenye vitu vya wanafunzi na vitanda, wanafunzi hawakuwepo bwenini, walikuwa wameenda msikitini kwa ajili ya swala ya jioni, mpaka sasa hivi tunaendelea na uchunguzi wa moto huo ili kubaini chanzo na moto ulipoanzia,” amesema Inspekta Abraham.

Aidha ameongeza kuwa, “Hapa wanafunzi wako katika hali ya mshtuko, mikakati iliyopo tunakagua shule moja baada ya nyingine kwa kushirikiana na vyombo vingine.

“Hata hii iliyoungua tunavyozungumza imekaguliwa juzi tu hata wiki haijaisha, lakini bahati mbaya imeungua, vyanzo vya moto viko vingi,  kuna umeme, hujuma, kuna vingine vinasababishwa kwa makusudi”.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post