Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Magufuli ameahidi kumaliza kero ya mafuriko jijini Dar es Salaam endapo akichaguliwa kuongoza kwa muhula wa pili.
Dkt. Magufuli ametoa ahadi hiyo jana wakati akizingumza na maelfu ya wakazi wa jijini hilo waliojitokeza katika Uwanja wa Tanganyika Packers wakati akihitimisha kampeni zake kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema kwa kushirikiana na wabunge na madiwani wa CCM ambapo watachaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, atahakikisha wanaboresha miundombinu ili mvua zinaponyesha, kusiwe na mafuriko.
Mbali na hilo ameahidi kuboresha huduma za afya, ujenzi wa viwanda, ajira kwa vijana, na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwani Dar es Salaam ni kitovu cha uchumi wa Tanzania.
Dkt. Magufuli amehitimisha kampeni zake kwa mkoa wa Dar es Salaam. Hata hivyo amewaomba radhi wakazi wa baadhi ya mikoa ambayo hatoweza kufika kwani licha ya kuwa kwenye kampeni, bado anatakiwa kuiendesha serikali.