DR MAGUFULI AAHIDI KUPANDISHA MISHAHARA KWA WATUMISHI
Tuesday, October 20, 2020
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dkt. John Magufuli leo Oktoba 20, 2020, amefanya mkutano katika uwanja wa TTC Korogwe mkoa wa Tanga leo na kunadi sera za chama hicho na kuomba ridhaa ya wana CCM, na wananchi kumchagua kuwa Rais na kuchagua wabunge na madiwani wa CCM.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Dkt. Magufuli ameahidi kupandisha mishahara kwa watumishi iwapo atapewa ridhaa hiyo huku akisisitiza kuwa ili mipango mbalimbali iweze kufanikiwa ni lazima kujipanga kukusanya fedha na kutengeneza miundombinu.
“Maendeleo ni lazima yapangwe, bila kupangwa hakuna kitakachofanyika. Miaka mitano ilikuwa ya kujipanga ndio maana tulijenga vituo vya afya, zahanati, hospitali za mikoa, rufaa lakini tukaongeza bima, bajeti ya madawa kutoka Sh31 bilioni hadi Sh270 bilioni, hayo yalikuwa maandalizi.
“Uongozi ulio makini ni lazima upange maandalizi, bila hivyo itakuwa ahadi hewa. Ndio maana tulipoingia madarakani tu tuliongeza kukusanya fedha kutoka Sh850 bilioni hadi Sh1.5 trilioni, na hii ndio imetusaidia kujenga reli ya kisasa ambayo tunatumia Sh7.2 trilioni, pia tumeanza mradi wa umeme wa Julius Nyerere,” amesema Magufuli.
Ameongeza, “Miaka mitano iliyopita, tumeajiri watumishi 74,000, tumeimarisha uchumi wetu, sasa miaka mitano ijayo tutakuwa na jukumu la kuongeza misharaha, huwezi kupandisha mishahara wakati huna uchumi, wengine wanazungumza tu hawajawahi kutawala, hata kujenga ofisi za chama zimewashinda."
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin