Mataifa ya kundi la G20 yamekubaliana kurefusha kwa miezi sita muda wa kulipa madeni kwa mataifa maskini yaliyoathiriwa na janga la virusi vya corona .
Wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya video, mawaziri wa fedha na magavana wa kundi la G20 wameridhia kusogeza mbele hadi Juni 2021 muda wa mwisho kwa mataifa masikini kuanza tena kulipa madeni yake ili kuzisaidia nchi hizo kupambana na janga la COVID-19.
Usimamishaji wa kulipa madeni ulikuwa unafikia tamati mnamo mwezi Novemba mwaka huu na kundi la G20 limesema muda wa nyongeza uliokubaliwa jana unaweza kurefushwa tena wakati wa majadiliano yatakayofanyika wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2021.
Waziri wa fedha wa Saudi Arabia Mohammed al-Jadaan aliyekuwa mwenyeji wa mkutano hwa G20 amesema ingawa uchumi wa dunia unaimarika taratibu, mataifa masikini bado yanakabiliwa na hali mbaya kutokana na athari za janga la COVID-19