Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wote kuheshimu sheria na taratibu za Uchaguzi kama zilivyoainishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, katika kikao kati ya viongozi wa vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambacho kililenga kuangalia na kutathimi mwelekeo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020, zinazoendelea sehemu mbalimbali nchini
“Hiki si kikao cha kuja kusutana ila ni kikao cha kuja kuongea na kuangalia mwelekeo unavyokwenda kwenye kampeni, lakini pia nafasi ya Msajili kama mlezi nikaona nisiwanyime hiyo nafasi ya kukutana nanyi na kuwapa maneno mawili ya kuwakumbusha wajibu wenu” Amesema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi amewaomba wagombea pamoja na wadau wa vyama vya siasa kuimarisha Demokrasia ya nchi kwa kufanya siasa za kistaarabu ambapo amewataka wagombea washindane kwa ustaarabu huku wakifuata sheria na taratibu za nchi.
Aidha ameeleza kuwa mtu yoyote atakayeonekana kwenda kinyume na maelekezo na taratibu za Uchaguzi atachukuliwa hatua kulingana na taratibu zilizowekwaza uchaguzi Mkuu 2020
“Tuachane na ile dhana ya kwamba mtu anasema wakiniacha wananiogopa, wakinishughulikia wananionea, sasa huu ujumbe ninaousema uende pande zote, na sisi taasisi ambazo zimepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa hii sheria, tuisimamie kwa haki kwa sababu tusipofanya hivyo tunaweza sababisha tafarani” Alisema Jaji Mutungi
Naye, Mwenyekiti wa women fund Tanzania Prof. Ruth Meena amewataka wagombea wote nchini wachukue wajibu wa kuzifahamu sheria na maadili ya uchaguzi ili waweze kuzijua haki zao, kutengeneza hoja za msingi na kuepuka kutumia lugha za matusi katika kampeni zao
“Wagombea ni lazima wachukue wajibu wa kuzielewa sheria, waelewe maadili ya Uchaguzi hasa yale yanayohusu haki za wanawake na vijana katika kushiriki kikamilifu”. Amesema Prof. Meena
Prof. Mena ameongeza kuwa wagombea wanawajibu mkubwa wa kujenga mazingira yatakayowezesha kutumia nguvu za hoja na si matusi wawapo katika kampeni zao ili kuweza kujenga mazingira ya amani.
Mwisho
Social Plugin