WAKAMATWA KWA TUHUMA YA KUMUUA BABA YAO


 UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA.

Mnamo tarehe 17.10.2020 majira ya saa 19:15 usiku huko eneo la RRM, Kata ya Isyesye, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya, ROSE RAULENT [30] Mfanyabiashara na Mkazi wa RRM akiwa nje ya geti la nyumba yake akitoka dukani kwake njia panda ya Ilomba alivamiwa na watu watatu wasiofahamika waliokuwa na silaha bunduki iliyotengenezwa kienyeji isiyokuwa na namba inayotumia risasi za Shotgun na kumtishia kisha kumpora mkoba uliokuwa na pesa takribani Milioni 5, simu 04 za mkononi na mashine 01 ya POS ya CRDB na kisha kutoweka na mali hizo.

Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na msako mkali dhidi ya watuhumiwa waliohusika kwenye tukio hili.

KUINGIA NCHINI BILA KUFUATA TARATIBU.
Mnamo tarehe 29/03/2020 majira ya saa 15 00 Alasiri huko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya, Jeshi la Polisi lilimkamata TEDDY NOAH MWAISEMBA [48] Mfanyabiashara na Mkazi wa Blantaya nchini Malawi wakati wa ukaguzi kabla ya kuingia kwenye ndege ya Air Tanzania kuelekea Dar es salaam.

Baada ya kumkamata na kufanya upekuzi alikutwa akiwa na:-

  •     Passport ya kusafiria ambayo haijagongwa muhuri kutoka Malawi na kuingia Tanzania,
  •     Dola za kimarekani (US Dollar) 30,000/=,
  •     Fedha za kitanzania Tshs 327,000/=.
  •     Nakala ya kitambulisho cha kupigia kura alichokipata mwaka 2014 kilichoandikishwa katika kituo cha Shule ya Msingi Magomeni Dar es salaam.


Katika uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ilibainika kuwa mtuhumiwa hapo awali alikuwa Mtanzania aliyekuwa akiishi Kimara Suka Dar es salaam na mwaka 2006 aliukana uraia wa Tanzania na kuchukua uraia wa Malawi kutokana na shughuli zake za biashara huku familia yake yote ikiwa Dar es salaam.

Kufuatia tukio hilo, taratibu za kumfikisha mahakamani zilifanyika ambapo mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya na alishtakiwa kwa makosa matatu ambayo ni:-

  •     Kuingia nchini au kuwepo nchini kinyume na sheria, kifungu cha 45(1) ( I) and ( 2) of immigration Act.CAP 54 R.E.2016.       
  •     Kumiliki kitambulisho cha mpiga kura kinyume na kifungu cha 11(1) (a) of the National Election Act CAP 343 R.E.2002,
  •     Kushindwa ku-declare currency kinyume na kifungu cha 5(1) and (5) cha sheria ya utakatishaji fedha ya mwaka 2016 na marekebisho yake ya mwaka 2012.


Mtuhumiwa alikiri makosa mawili na akalipa faini ya Tshs.600,000/= yaani Tshs.500,000/= kwa kosa la kwanza na Tshs.100,000/= kwa kosa la pili, huku kosa la tatu alikana lakini kwa ushahidi ulionyooka mtuhumiwa alitiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini milion 100 au jela miaka miwili. Mshtakiwa amelipa faini.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WATANO WA TUKIO LA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watano kati yao wanne wa familia moja ambao ni 1. CHAUSIKU MAHAMUDU [50] Mkazi wa Mbuyuni, 2. SADA ALI @ MAZINGE [28] Mkazi wa Ubaruku, 3. IDRISA ALI @ MAZINGE [24] Mkazi wa Mbuyuni 4. JUMANNE ALI @ MAZINGE [30] Mkazi wa Mbuyuni na FIKIRI ALLY @ RASI [38] Mkazi wa Mabadaga kwa tuhuma za mauaji ya baba yao aitwaye ALI HAMIS @ MAZINGE [66] Mkazi wa Mbuyuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Tukio hili lilitokea mnamo tarehe 25.06.2020 majira ya saa 21:00 usiku huko Kitongoji cha Mbuyuni, Kijiji cha Mpakani, Kata ya Ubaruku, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya ambapo CHAUSIKU MAHAMUDU [50] ambaye ni mke wa marehemu kwa kushirikiana na watoto wa marehemu walimuua baba yao akiwa amelala kitandani kwa kumkata kwa kitu chenye ncha kali sehemu ya taya la kulia na shingoni.

Awali mnamo tarehe 24.06.2020 majira ya asubuhi mke wa marehemu alimpatia fedha ya nauli mtoto wake aitwaye IDRISA ALI kwa ajili ya kwenda kumtafuta muuaji na ambaye ni FIKIRI ALLY @ RAS [38] Mkazi wa Mabadaga na mapema tarehe 25.06.2020 majira ya saa 09:00 asubuhi alifika naye hadi nyumbani kwa marehemu baba yao na kumuonyesha mazingira ya hapo nyumbani.

Mtuhumiwa FIKIRI ALLY alipohojiwa alikiri kutekeleza mauaji hayo baada ya kununuliwa na kuahidiwa atakapofanikiwa atapewa fedha taslimu Tshs.700,000/= ambapo baada ya tukio hilo kweli alikabidhiwa fedha hizo.

Chanzo cha tukio hili ni imani za kishirikina ambapo CHAUSIKU MAHAMUDU ambaye ni mke wa marehemu alikuwa anaumwa koo kwa muda mrefu kitendo ambacho kilimpelekea kwenda kwa mganga wa kienyeji aitwaye SADIKI TITU [40] Mkazi wa Usuka Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe ambapo baada ya kufika walipiga ramli chonganishi na kuambiwa kuwa maradhi yanayomsumbua msababishi mkubwa ni mume wake kwani anawaroga yeye [mke] pamoja na watoto wake. Pia ni mgogoro wa kifamilia kati ya marehemu na watuhumiwa ambao walikuwa wanataka baba yao kuuza eneo huku marehemu hakuwa tayari hivyo kufanya njama za kumuua.

Taratibu za kuwafikisha watuhumiwa mahakamani zinaendelea mara baada ya upelelezi kukamilika.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MATUKIO YA WIZI NA UPORAJI WA PIKIPIKI NA BAJAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia GORDEN LUKA @ KIDUMBA [23] Mfanyabiashara na MARIO TITO @ WIKESI [20] Mfanyabiashara wote wakazi  wa Ilembula kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi ambayo ni Pikipiki ya magurudumu matatu @ Bajaji.

Awali mnamo tarehe 11.10.2020 majira ya saa 20:30 usiku huko Kijiji cha Mdodela – Ubaruku, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya mwendesha Bajaji aliyefahamika kwa jina la YUSTINE MWIDUNDA [19] Mkazi wa Ubaruku aliporwa Bajaji yake yenye namba ya usajili MC.582 CBG aina ya TVS King yenye thamani ya Tshs.7,000,000/= na abiria watatu waliomkodi kutokea Igawa kwenda Ubaruku ambao baada ya kufika eneo la Mdodela waliomba kujisaidia kisha kumvamia na kumpora Bajaji hiyo na badae walimshusha na kumtelekeza karibu na vichaka vya Shule ya Msingi Mbarali.

Kutokana na tukio hilo, Kikosi kazi cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Njombe kilifanya msako huko Kijiji cha Ilembula, Kata ya Luduga, Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe na mnamo tarehe 14.10.2020 majira ya saa 11:00 asubuhi kilifanikiwa kuwatia nguvuni watuhumiwa wawili kuhusiana na tukio hilo.

Katika mahojiano na watuhumiwa walikiri kufanya tukio la uporaji Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili kubaini matukio mengine waliyoshiriki ya uporaji, mauaji ya bodaboda na kutaja washirika wengine.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA KOSA LA KUJERUHI KWA MOTO.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. EZEKIA LIZER [20] na 2. BARAKA EZEKIA [24] wote wakazi wa Tarafani Mji Mdogo wa Mbalizi kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kutumia moto DAINES ROBERT MDEE [26] Mkazi wa ZZK ambaye ni mama yao wa kambo kutokana na mgogoro wa mali za familia.

Tukio hili limetokea mnamo tarehe 18.10.2020 majira ya saa 06:00 asubuhi huko eneo la ZZK – Mbalizi, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya. Ni kwamba chanzo cha tukio hili ni mgogoro wa mali za familia zilizoachwa na mume wa mhanga baada ya kufariki dunia hivyo watoto wa marehemu [watuhumiwa] kumtuhumu mhanga kutumia hati za nyumba za marehemu baba yao kukopea pesa benki kiasi cha Tshs.Milioni 40 na baadae kuondoka  na kuacha Benki ikitaka kuuza nyumba hizo.

Kutokana na kitendo hicho, watuhumiwa walimvizia mama yao wa kambo wakati anaenda kufungua duka kisha kummwagia mafuta ya Petroli ujazo wa lita 10 yaliyokuwa kwenye ndoo na kisha kumchoma moto kwa kutumia kiberiti. Mhanga amelazwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matabibu. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post