Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya Azindua Maabara Mpya Ya Wakala Wa Mbegu Za Kilimo (Asa)
Wednesday, October 14, 2020
Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Musabila jana jioni, tarehe 13 Oktoba, 2020 amezindua maabara ya kisasa iliyojengwa kupitia Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji kwenye zao la Mpunga (ERPP) kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) mjini Morogoro.
Akizungumza kabla ya kuzindua maabara hiyo; Katibu Mkuu Gerald Musabila Kusaya amesema jengo la maabara hiyo ni moja ya kazi nzuri iliyofanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo na hatimaye maabara hiyo iko tayari kuanza kutumika.
Katibu Mkuu amesema licha ya kuizindua maabara hiyo; Kuna vifaa vingine ambavyo vinapaswa kununuliwa ili kuiwezesha maabara hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na kwamba Wizara itanunua vifaa hivyo mapema iwezekanavyo.
Katibu Mkuu Kusaya amesema suala la kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo ndiyo limesukumu sehemu kubwa ya mabadiliko ya kiutendaji katika maeneo mbalimbali ambapo; Ili taifa liongeze uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula yanaenda sambamba na matumizi ya mbegu bora pamoja na pembejeo nyengine.
“Suala la kuongeza uzalishaji wa mbegu bora ni suala la msingi hasa kipindi hiki ambacho mahitaji na matumizi ya mbegu bora za kilimo, yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, bado kasi ya uzalishaji wa mbegu ni ndogo.”
Aidha; Katibu Mkuu ametoa rai kwa Watumishi wa Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo kuendelea kutoa huduma ya kuzalisha mbegu bora za mazao ya kilimo licha ya kukabiliana na changamoto kadhaa.
“Nafahamu changamoto nyingi zilizopo na mnazopitia kama Wakala wa Serikali lakini bado mnahitaji kuongeza juhudi, kasi na ufuatiliaji ulio makini katika suala zima la uzalishaji wa mbegu bora ili ziwafikie na kubadilisha maisha ya wakulima wetu. Dhamana hii mliyopewa ni kubwa na usimamizi wake lazima uendane na kufanya kazi kwa kujituma na kwa uadilifu wa hali ya juu. Kufanya kazi ASA ni sawa na kufanya kazi benki kwani fedha zipo na unazishika kila siku lakini sio zako.” Amekaririwa Katibu Mkuu.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kusaya ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Watumishi wa Wakala wa Mbegu Bora (ASA) kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uhadilifu mkubwa.
“Ndugu zangu, napenda niwahimize kila Mtumishi afanye kazi kwa uhamimifu mkubwa; Binafasi uwa nachukia sana wizi wa mali za umma, matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Niwaomba tufanye kazi na atakayekataa kufanyakazi kwa uadilifu; Tutamchulia hatua.
Baadae Katibu Mkuu alielekea kwenye kuzindua rasmi maabara hiyo kwa kukata utepe kama ishara ya kuzinduliwa rasmi kwa jengo hilo la maabara.
Baadae Katibu Mkuu alikabidhi matrekta makubwa mawili kwa ajili ya kuongeza eneo la kilimo cha mashamba ya ASA. Matrekta hayo yana uwezo wa HP 95 na ni aina ya Valtra kutoka nchini Brazil yote yakiwa na thamani ya shilingi milioni 273.6. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo, Dkt. Sophia Kashenge amesema kuongezeka kwa matrekta hayo mawili; Kunaifanya ASA kuwa na matrekta matano (5) na kwamba matrekta hayo; yatachangia katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora mara dufu.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin