Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba (kulia), kushoto ni mfano wa kisu cha moto
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la
polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Meckrida Masesa (25), mkazi wa Chela wilayani Kahama kwa kosa la kumjeruhi mdogo
wake mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa), mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya
Sekondari Baloha kwa kumuunguza sehemu za usoni, mashavuni na mapajani kwa
kutumia kisu cha moto akimtuhumu kuchepuka na shemeji yake.
Kwa Mujibu
wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba tukio hilo
limetokea Septemba 28,2020 majira ya saa kumi na moja jioni katika kijiji na
kata ya Chela, halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama.
Amesema mhanga alijeruhiwa kwa kuunguzwa na kisu cha moto na mtuhumiwa huyo ambaye ni
dada yake wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa.
“Chanzo
kikiwa ni wivu wa mapenzi baada ya dada yake huyo kumtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na shemeji
yake ambaye ni mume wa mtuhumiwa huyo aitwaye Joseph Masolwa ambaye ni mwalimu
wa shule ya msingi Chela”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
“Mtuhumiwa
alikiweka kisu hicho kwenye moto kwanza na kisha kuanza kumjeruhi
mhanga. majeruhi anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Lunguya na hali
inaendelea vizuri”,amesema.
Kamanda Magiligimba
anatoa wito wenzi/wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala
wapeleke matatizo/migogoro yao ya ndoa kwenye ofisi za dawati la jinsia na
watoto, viongozi wa dini,ofisi za ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao.