KIWANJA CHA NDEGE SONGEA KUBEBA NDEGE KUBWA SITA KWA WAKATI MMOJA,SASA NDEGE KUTUA SAA 24
Wednesday, October 21, 2020
SERIKALI ya awamu ya tano imetenga kiasi cha shilingi bilioni 37 kukarabati uwanja wa ndege wa Songea ambao utawezesha kwa wakati mmoja kubeba ndege sita aina ya bombardier.
Akitoa taarifa ya ukarabati wa kiwanja hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme,Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Songea Jordan Mchami,amesema kazi ya ujenzi wa barabara ya kutua ndege yenye urefu wa meta 1740 na upana wa meta 30 imeshakamilika.
Amesema ujenzi wa maegesho ya ndege yenye ukubwa wa meta 139 kwa 126 ipo kwenye hatua za mwisho kukamilika na inatarajia kukamilika katikati ya mwezi Novemba mwaka huu hivyo kumudu kuegesha ndege kubwa zaidi ya sita.
Meneja huyo wa Kiwanja cha ndege Songea amesema pia yamejengwa maegesho maalum ya kuegesha ndege za dharura yenye ukubwa wa meta 70 kwa 40 na kwamba katika kiwanja hicho zimejengwa taa za kisasa za kuongozea ndege wakati wa usiku hivyo kuwezesha ndege kutua saa 24 yaani usiku na mchana.
“Ndege aina ya bombardier sasa zitaanza kutua wakati wowote katika kiwanja cha ndege cha Songea,tunatarajia ndege ya kwanza itatua kabla ya mwisho wa mwezi huu Oktoba’’,alisema Mchami.
Amesema jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria 150 kwa wakati mmoja limejengwa na kukamilika katika uwanja wa ndege wa Songea hali ambayo inaweza kumudu abiria wa ndege mbili za bombardier kwa wakati mmoja.
Amesema gharama za nauli katika ndege hizo za serikali zitakuwa chini ukilinganisha na ndege ndogo za watu binfasi ambazo nauli yake ni kati ya shilingi 500,000 hadi 600,000 hali ambayo wananchi wengi hawawezi kumudu.
Amesema ujio wa ndege ya bombardier utakuwa ni ukombozi kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa sababu wananchi watalipa shilingi 400,000 toka Songea hadi Dar es salaam, kwenda na kurudi.
Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati wa uwanja huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Kampuni ya CHICCO ambayo inakarabati kiwanja hicho,ambacho ukarabati wake unatarajia kukamilika kwa asilimia 100 Desemba mwaka huu.
Mndeme amesema kiwanja cha ndege wa Songea ni rasilimali adimu inayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea na Mkoa mzima wa Ruvuma hasa kukuza sekta ya utalii,baada ya kuanzishwa mpango mkakati wa kukuza utalii katika mkoa wa Ruvuma.
Kiwanja cha ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja bora vya ndege Tanzania ambacho kilijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 na kiliwekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote masika na kiangazi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin