MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ijayo ya CCM itaanzisha maabara na kliniki za kutibu mifugo katika wilaya zote za wafugaji nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Oktoba 16, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Orgosorok, wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Waziri Mkuu, mji mdogo wa Loliondo.
“Tumeanza kuwatumikia na kuwahudumia wafugaji kwa kuhakikisha kuwa wana maeneo mazuri ya malisho, na sasa tumeamua kuwachimbia mabwawa ya kunywesha mifugo. Bado tutaendelea kubaini maeneo ya wafugaji na kuwachimbia mabwawa na majosho. Na sasa, tunaanzisha maabara kwa ajili ya kupima magonjwa ya mifugo. Tunajenga kliniki kwa ajili ya kutibu mifugo kwenye wilaya zote zinazofuga na pia tunatoa dawa ya ruzuku kwa ajili ya mifugo.”
Amesema Serikali ya CCM itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuhudumia mifugo na hivyo, wafugaji waendelee kufuga kwa uhakika ili Watanzania wanufaike na sekta ya mifugo.
Kuhusu barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ijayo ya CCM itajenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa km. 300 kutoka Mto wa Mbu hadi Ngorongoro.
Mheshimiwa Majaliwa amewaomba wananchi wa Ngorongoro wamchangue tena Dkt. John Magufuli ili aendelee kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ameonesha uwezo mkubwa katika kukusanya mapato ya Serikali na kusimamia matumizi yake.
Amesema: “Kazi ya Urais ni kazi nzito na haina nafasi ya kufanyiwa majaribio na mtu ambaye hana historia na uongozi wa nchi,” na kusisitiza kuwa: “Amani ya nchi inategemea kwa kiwango kikubwa na kiongozi aliyeko madarakani, kwani akiwa kiongozi mahiri ataisimamia amani iliyopo, na akiwa kiongozi legelege amani itayumba.”
Wakati huohuo, Mama Mary Majaliwa amewaomba wakazi wa Ngorongoro wampe kura zote za ndiyo Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Ngorongoro Bw. William Ole Nasha na wagombea udiwani wote kwa tiketi ya CCM.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Ngorongoro kwa tiketi ya CCM, Bw. William Tate Ole Nasha amesema maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha awamu ya kwanza ya miaka mitano ya Dkt. Magufuli ni makubwa na hakika historia ya maendeleo imeandikwa katika wilaya ya Ngorongoro.
“Kwa mara ya kwanza, Chuo cha ufundi VETA kinajengwa Ngorongoro na Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho katika eneo la Samunge, Loliondo”
Pia Bw. Ole Nasha amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwani wananchi wa Ngorongoro hawatalazimika kwenda Arusha au nchi jirani ili kupata matibabu.
Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Arusha kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Ngorongoro William Ole Nasha na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM.
(mwisho)