MAJALIWA: KIWANDA CHA CHAI MPONDE KUANZA UZALISHAJI
Saturday, October 10, 2020
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa chai wilayani Lushoto wajiandae na kilimo hicho kwa kuwa kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo katika jimbo la Bumbuli kinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Kiwanda cha chai Mponde ni miongoni mwa viwanda vya kusindika majani mabichi ya chai katika Halmashauri ya Bumbuli na hutegemewa na wakulima wadogo wa chai wapatao 5,000 kama soko la majani mabichi ya chai kutoka katika mashamba yao, ambapo uzalishaji ulisimama kufuatia mgogoro uliojitokeza mwaka 2013.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Oktoba 9, 2020) alipozungumza na wananchi wa jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto, Tanga katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Soni wakati alipomuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea udiwani baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo January Makamba kupita bila ya kupingwa.
“Najua msimu huu mmehangaika sana, lazima kiwanda chetu kianze kazi na hatua zote za msingi zimeshakamilika. Msimamizi mkuu ni Msajili wa Hazina na mwekezaji ni mifuko ya hifadhi ya jamiii ya PSSSF na WCF, ambao walishakuja kufanya ukaguzi ila kuna mitambo inahitaji vipuri na tumeagiza vichongwe ili kazi ianze chai isindikwe.”
Alisema mitambo ile ni ya miaka mingi sana na hata teknolojia yake imepitwa na wakati, hivyo kwa sasa wameagiza vipuri vichongwe ili chai ya wakulima iendelee kusindikwa wakati wawekezaji hao wakitafuta mashine nyingine mpya na za kisasa ambazo zitakapopatikana zitabadilishwa huku zoezi la usindikaji likiwa linaendelea.
Mheshimiwa Majaliwa alisema mpango wa kibiashara (Business Plan) wa kukarabati kiwanda hicho uliandaliwa na umeshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kama sehemu ya matakwa ya wizara ili kuridhia matumizi ya fedha kutoka kwenye mifuko hiyo kiasi cha shilingi bilioni 4.05 kwa ajili ya ukarabati na uendeshaji wa kiwanda.
Alisema zao la chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati hapa nchini na Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo pamoja na kutatua changamoto ya masoko kwa sababu zaidi ya asilimia 85 ya chai inayozalishwa hapa nchini huuzwa nje ya nchi na kiasi kinachobakia huuzwa kwa makampuni yanayochanganya na kufunga chai kwenye vikasha (Blenders and Packers).
Mheshimiwa Majaliwa alisema kufuatia uwepo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayasababishwa na virusi vya corona, baadhi ya masoko ya chai ndani na nje ya nchi yaliathirika hali iliyosababisha kushuka kwa bei ya chai kwenye masoko na baadhi ya makampuni kushindwa kulipa wakulima wadogo kwa wakati.
“Pamoja na kushuka kwa wastani wa bei ya chai ya Tanzania katika masoko ya nje, bei elekezi ya majani mabichi ya chai kwa wakulima wadogo iliendelea kubakia shilingi 314 kwa kilo na haikushuka, athari kubwa kwa wakulima wadogo ilikuwa ni kukosa malipo ya pili ambayo hupatikana kutegemeana na ufanisi wa kiwanda katika soko la chai.”
Alisema kwa sasa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kwa kushirikiana na Bodi ya Chai Tanzania wanakamilisha taratibu za uanzishwaji wa mnada wa chai hapa nchini, ambao unatarajiwa kuvutia wanunuzi kutoka sehemu mbali mbali duniani. Bodi ya Chai imeshafanya jitihada za kutafuta wanunuzi ikiwa ni pamoja na kukutana na Ubalozi wa Pakistani ili kuweza kupata orodha ya wanunuzi wakubwa kutoka katika nchi hiyo.
Uanzishwaji wa mnada wa chai hapa nchini utatoa fursa kubwa kwa wazalishaji wa chai ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo kuongeza uzalishaji kwani changamoto ya ucheleweshwaji wa malipo itakuwa haipo na litaboresha uwazi katika biashara ya chai hali ambayo itachangia katika kuboresha bei na mapato ya mkulima mdogo wa chai.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ameelezea dhamira ya Serikali ya kuboresha kilimo cha mbogamboga na imepanga kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje ya mbogamboga kwa zaidi ya maradufu ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika kuboresha kilimo hicho ni pamoja na kujenga vituo vya kuchakata na kuhifadhi mazao ya bustani (industrial packs) katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Songwe, kujenga vituo vya kuchakata na kuhifadhia mazao katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Kigoma, Manyara, Mara, Mbeya, Tabora, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Singida, Shinyanga, Songwe, Tanga, na Katavi.
Mheshimiwa Majaliwa Alisema tayari Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilishajenga soko lenye chumba maalumu cha baridi kwa ajili ya kuhifadhia mazao hayo wilayani Lushoto na sasa inaendelea na uchimbaji wa mabwawa ili yaweze kutumika kwa umwagiliaji. “Mna fursa za kibiashara zinazoboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kupitia kilimo kwani hata Dar es Salaam wanategemea mbogamboga kutoka Lushoto.”
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin