MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Masasi watambue kwamba nafasi ya urais inagusa maisha yao na wala si jambo la mchezo.
“Wazee wangu, mama zangu na vijana wenzangu, urais siyo jambo la mchezo, urais ni maisha yako wewe. Urais wa Tanzania unataka mtu mwenye uwezo wa kuongoza watu zaidi ya milioni 60 wenye dini, vyama, makabila, na uwezo tofauti,” amesema.
Ametoa wito huo jana (Jumatano, Oktoba 21, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Masasi katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba kata ya Mkuti, wilayani Masasi, mkoani Mtwara.
“Leo usije ukachagua mtu anayeendekeza mambo ya udini, utakuwa umefanya kosa kubwa sana. Nchi hii imejengwa kwa misingi na uadilifu, hatuangalii kabila au dini ya mtu, kipato cha mtu au rangi ya mtu,” amesisitiza.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mtwara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Masasi, Bw. Godfrey Mwambe; mgombea ubunge wa jimbo la Ndanda, Bw. Cecil Mwambe; mgombea ubunge wa jimbo la Lulindi, Bw. Issa Ally Mchungaela na wagombea udiwani wa CCM.
“Tunataka kiongozi atakayehubiri amani, tunataka kiongozi ambaye tuna historia naye, tuache kufanya uchaguzi kwa kufuata upepo. Tunataka kiongozi ambaye ataleta maendeleo. Tumchague Rais, narudia tumchague Rais, tusichague mtu wa kwenda kukaa Ikulu,” amesisitiza.
Mapema, akiwa njiani kuelekea Masasi, Mheshimiwa Majaliwa alisimamishwa na wakazi wa vijiji vya Chienjele, Namakuku na Mibura katika kata ya Chienjele, wilayani Ruangwa ambako aliwaomba wakazi hao ifikapo Jumatano ijayo, (Oktoba 28) wampigie kura za ndiyo mgombea urais wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli.
Mbunge wa jimbo la Ruangwa, Kassim M. Majaliwa na diwani wa kata hiyo, Bw. Rashid Nnunduma, wote wamepita bila kupingwa.
Aliwaeleza wakazi hao kwamba kiasi cha sh. bilioni 58 kimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa kwa kiwango cha lami. “Fedha imeshatolewa, mkandarasi wa Kichina ameshaanza kazi kutoka Namahema kwenda Nanganga na naamini watakamilisha kazi yao ifikapo Agosti, 2021 kama walivyoahidi,” amesema.
Alisema barabara ya kutoka Namahema na Nandangala kuelekea Makutano – Nachingwea nayo pia itajengwa kwa kiwango cha lami. Alisema miradi ya maji inaendelea kujengwa ili kuwaondolea adha wakazi hao na akawaomba wamchague Rais Magufuli ili akamilishe kazi aliyoianza.