Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza masikitiko yake kuhusu kauli ya mgombea urais kupitia chama hicho, Bernard Membe kutangaza kuendelea na kampeni wakati chama hicho kimetangaza kumuunga mkono mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.
Maalim Seif ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akijibu kauli ya Membe ambaye jana katika mkutano wake na wanahabari aliahidi kuendelea na kampeni siku nane zilizobaki kabla ya uchaguzi mkuu
Membe alifanya mikutano mitatu ya kampeni kati ya Agosti 26 na Septemba 3, 2020 kwenye mikoa ya Pwani na Mtwara na tangu kipindi hicho hajawahi kuonekana jukwaani hadi alipoibuka jana na kueleza kwamba atafanya kampeni za lala salama.
“Membe alipokuja tulimwambia uamuzi wa mkutano mkuu ni tushirikiane na vyama vingine. Tukamuuliza tukiamua kushirikiana utakubali? Akasema ‘Naam.’ Tulipoona kampeni zetu zimesuasua, tukaamua, na Membe akiwepo, tumuunge mkono Tundu Lissu.
“Mgombea wetu (Bernard Membe) haonekani. Ni afadhali mzee wa ubwabwa (Hashim Rungwe) anaonekana. Kamati ya uongozi kwa kauli moja pamoja na Membe tulikubaliana tumuunge mkono Tundu Lissu. Siyo kwamba hatumpendi Membe.
“Alilosema Zitto Kabwe si lake! Nililosema mimi Maalim Seif si langu! Bali ni maamuzi ya chama. Ni msimamo wa ACT Wazalendo .Mimi nam-challenge, afanye hizo kampeni zake tuone hizo kampeni ziko wapi. Nia yake ni kutaka kuwachanganya Watanzania."- Amesema